Boresheni huduma kwa wananchi, msiridhike na ubora wa majengo!
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa majengo
mazuri ya ofisi za Halmashauri mbali mbali nchini ni muhimu lakini muhimu zaidi ni
wafanyakazi na watumishi wa halmashauri hizo kuwa waaminifu na waandilifu katika utumishi
wa umma. Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa ni wajibu wa watumishi wa halmashauri nchini
kupunguza manung’uniko na malalamiko ya wananchi kwa kutimiza ipasavyo wajibu wao
wa kutumikia wananchi.
Rais Kikwete ameyasema hayo Jumapili, Oktoba 20, 2013,
wakati alipoweka jiwe la msingi kwenye Ujenzi wa Jengo la Halmashauri ya Mji wa Njombe
kwenye eneo la Mji Mwema, nje kidogo ya mji wa Njombe. Rais Kikwete ambaye yuko katika
ziara ya siku saba ya kikazi katika Mkoa wa Njombe amewaambia wananchi na viongozi
waliohudhuria sherehe hizo ya kuweka jiwe la msingi:
“Nawapongezeni kwa kujenga
jengo zuri na jipya kama hili. Linaongeza heshima kwa mji wa Njombe ambao ni makao
makuu ya Mkoa wa Njombe. Lakini ubora wa jengo pekee hautoshi kwa utumishi bora wa
wananchi,” amesema Rais Kikwete na kuongeza: “Ubora wa utumishi wa wananchi utapatikana
tu endapo watumishi wa halmashauri hii na nyingine zote nchini watakaofikia kiwango
cha kufanya kazi kwa uaminifu, uadilifu,wenye tija na matunda ya dhahiri kwa wananchi.”
Rais
Kikwete amesema kuwa moja ya wajibu mkubwa wa watumishi wa halmashauri na wa umma
kwa jumla nchini ni kupunguza malalamiko na manung’uniko ya wananchi kwa kuboresha
kiwango cha ubora wa utumishi wao.