2013-10-19 07:30:29

Tamaa ya utajiri wa harakaharaka ni chanzo cha kukomaa kwa biashara haramu ya dawa za kulevya!


Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema katika kipindi alichokaa ofisini na kushughulikia suala la dawa za kulevya amebaini kuwa tatizo la biashara na matumizi haramuya dawa hizo linakuzwa kwa kiasi kikubwa na hulka ya watu kutaka kupata utajiri wa haraka.

Ametoa kauli hiyo Ijumaa, Oktoba 18, 2013 wakati akizungumza na Watanzani waishio jijini Beijing, China alipokutana nao kwenye ubalozi wa Tanzania nchini China. Waziri Mkuu alikuwa katika siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi ya siku tisa kwa mwaliko wa Serikali ya nchi hiyo.

Amesema wahusika wa biashara hiyo wana siri kubwa na wanakula kiapo kwani wengi wao wako tayari kufa lakini hawako tayari kuwataja wale waliowatuma kupeleka mizigo yao.

“Biashara hii imetawaliwa na usiri mkubwa... watu hawako tayari kutajana. Wako radhi kufa. Changamoto tuliyonayo ni kuangalia kwa namna gani tunaweza kupunguza shauku hii ya matumizi ya dawa za kulevya,” alisema.

Waziri Mkuu alikuwa akijibu swali lililoulizwa na Bi. Fatma Matulanga ambaye yuko masomoni nchini China kutaka kujua ni hatua gani ambazo Serikali imechukua kuhusiana na suala la vijana 175 waliokamatwa nchini China yakiwemo makosa ya kukutwa na dawa za kulevya ambayo adhabu yake ni kifo.

Alisema kama taratibu zinaruhusu, maafisa walioko ubalozini wafanye jitihada ya kuonana na vijana hao na kuwasikiliza ili waweze kuona namna gani ya kupata taarifa sahihi na kama wako tayari kuwataja wale waliowatuma.

Awali, Waziri Mkuu alielezwa na Bi. Matulanga kwamba balozi aliyekuwepo China, Bw. Philip Marmo aliahidi kutuma viongozi wa dini kwenye magereza hayo ili wawasikilize vijana hao na kuona wanaweza vipi kuwasilisha taarifa zao Serikalini.

Alisema Rais Jakaya Kikwete aliunda kikosi maalum cha kudhibiti dawa za kulevya ambacho kimekuwa kikifanya kazi nzuri. Alitoa rai kuwa endapo kuna mtu ana taarifa zozote ama kuwafahamu watu wanaojihusisha na biashara hiyo, apeleke taarifa kwenye kikosi hicho nao watafanya uchunguzi wa kina ili kubaini ukweli na hatua stahiki zitachukuliwa.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaeleza Watanzania hao wa ughaibuni hatua mbalimbali za kisiasa na kiuchumi ambazo nchi imepitia katika siku za hivi karibuni. Pia aliwagusia kuhusu mchakato wa kupata Katiba mpya na hatua iliyofikiwa.








All the contents on this site are copyrighted ©.