2013-10-19 14:28:01

Papa Francisko kuungana na familia kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuadhimisha Mwaka wa Imani hapo tarehe 27 Oktoba 2013


Baada ya Baba Mtakatifu Francisko kufanya hija ya kichungaji mjini Assisi, kushiriki na waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia katika mkesha na Ibada ya Misa Takatifu kwa heshima ya Bikira Maria wa Fatima, kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani; Jumapili tarehe 27 Oktoba 2013, Baba Mtakatifu ataungana na familia kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwa ajili ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa ajili ya familia.

Hii itakuwa ni siku maalum kwa ajili ya Mama Kanisa kutafakari dhamana na utume wa Familia ndani ya Kanisa na Jamii kwa ujumla, mada itakayofanyiwa kazi wakati wa Maadhimisho ya Sinodi Maalum kwa ajili ya Familia hapo Oktoba 2014.

Ratiba ya Maadhimisho ya Ibada za Kipapa iliyotolewa h ivi karibuni na Mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa Monsinyo Guido Marini inaonesha kwamba, hapo tarehe Mosi, Novemba, 2013, Siku kuu ya Watakatifu wote, Baba Mtakatifu Francisko, majira ya jioni anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye makaburi ya Verano kwa jili ya mji wa Roma.

Tarehe 2 Novemba, 2013, Kumbu kumbu ya Marehemu Wote, Baba Mtakatifu atatembelea Makaburi ya Mapapa yaliyoko chini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kusali huko. Na tarehe 4 Novemba, 2013, asubuhi, Baba Mtakatifu ataongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Makardinali na Maaskofu waliofariki dunia katika kipindi cha Mwaka 2012-2013.

Tarehe 24 Novemba 2013, Siku kuu ya Kristo Mfalme wa Ulimwengu, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuungana na Familia ya Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwa ajili ya kufunga rasmi Mwaka wa Imani, uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI. Ibada ya Misa Takatifu inatarajiwa kuanza saa 4:30 kwa Saa za Ulaya. Kama kawa, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, itakula nawe "sahani moja" ili kukujuza yale yanayoendelea kujiri katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu.

Ukiwa na haraka zako, usikose kuchungulia katika mtandao wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vaticahn, hapo utatukuta tumejaa tele kama pishi la mchele!







All the contents on this site are copyrighted ©.