Mwenyeheri Stefano Sàndor ni mfano wa uaminifu kwa wito wa Kikristo, majitoleo ya
elimu kwa vijana na majiundo makini ya Kikristo!
Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa
wenyeheri na watakatifu, Jumamosi, tarehe 19 Oktoba 2013, kwa niaba ya Baba Mtakatifu
Francisko amemtangaza Mtumishi wa Mungu Stefano Sàndor, mwamini mlei wa Shirika la
Wafranciskani wa Sale kuwa Mwenyeheri, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika
kwenye jimbo kuu la Budapest, nchini Hungaria.
Mwenyeheri Stefano Sàndor aliyeishi
kati ya mwaka 1914 hadi mwaka 1953, alizaliwa na kuishi katika familia iliyokuwa imejikita
katika misingi ya Kikristo. Ni mtu aliyeishi katika kipindi kigumu cha historia ya
Hungaria. Daima alikuwa ni mwamini aliyependa kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu,
katika Parokia iiliyokuwa inaongozwa na Ndugu wadogo wa Mtakatifu Francisko.
Tangu
ujana wake, alitambua umuhimu wa dini na tunu msingi za maisha ya kibinadamu, mambo
yaliyomfanya kujisikia kuwa na wito wa kujiunga na Wasalesiani wa Mtakatifu Bosco.
Alijikita katika majiundo endelevu yaliyokuwa yanatolewa na Wasalesiani.
Madhulumu
ya kidini nchini Hungaria kunako mwaka 1949, yalipelekea mali nyingi ya Kanisa kutaifishwa
na waamini na watawa wakakumbana na "ufagio wa chuma", hali iliyowafanya wengi wao
kukimbilia uhamishoni au kuishi katika hali ya uficho. Stefano naye akajikuta anaikimbia
nchi yake kwa kuhofia usalama wa maisha yake anasema Kardinali Angelo Amato. Baadaye
alipata ujasiri wa kuendelea kazi yake ya uchapishaji, ingawa alitambua kwamba, ilikuwa
imepigwa rufuku na utawala wa kinazi.
Tarehe 28 Julai 1952, Polisi ikamtia
pingu mikononi na kupelekwa gerezani, alikoteswa na kunyanyaswa kutokana na imani
yake kwa Kristo na Kanisa lake. Akapandikiziwa mashitaka kwamba, alikuwa na mpango
wa kutaka kuipindua serikali na hatima yake ni kuhukumiwa kifo, adhabu iliyotekelezwa
hapo tarehe 8 Juni 1953. Kunako mwaka 1990 adhabu ya kifo aliyopewa Stefano ikafutwa
na akapewa nishani maalum na Serikali ya Hungaria.
Mwenyeheri Stefano ameliachia
Kanisa mambo makuu matatu: Uaminifu kwa maisha na wito wa Mkristo hadi kifo; mwendelezo
wa mchakato wa elimu kwa vijana na majiundo makini ya Kikristo, ili hatimaye, kuweza
kuishuhudia imani kwa njia ya matendo. Waamini watambue kwamba, Injili ni chemchemi
ya imani, matumaini na mapendo.
Hii ni changamoto kwa Mama Kanisa kuendelea
kuwekeza katika majiundo ya vijana wa kizazi kipya anasema Kardinali Angelo Amato,
ili kupambana na utamaduni mamboleo unaosigana na tunu msingi za maisha ya kiutu,
kimaadili na kijamii; mwelekeo potofu dhidi ya upendo, bidii ya kazi, msamaha na
udugu.