Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita, ICC, mwishoni mwa juma, imetoa
msamaha kwa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya anayekabiliwa na mashitaka ya mauaji ya watu
zaidi ya 1200 yaliyotokea kunako mwaka 2007 mara baada ya uchaguzi mkuu nchini Kenya
kwamba, kwa sasa hatalazimika tena kuwepo wakati wote Mahakamani hapo wakati wa kusikiliza
kesi yake inayomhusisha pia Makamu wa Rais wa Kenya Bwana William Ruto. Kesi hii inatarajiwa
kuendelea kusikilizwa tena, mwezi Novemba, 2013.
Uamuzi huu ni matokeo ya shinikizo
kutoka kwa viongozi wa Umoja wa Afrika ambao wamekuwa wakitishia kujitoa katika Mahakama
hii kutokana na ICC kuendelea kuwakandamiza viongozi kutoka Afrika, hali ambayo ingegumisha
mchakato wa mapambano dhidi vitendo vya kigaidi Barani Afrika. Hivi karibuni nchi
za Magharibi zilimshauri Rais Uhuru Kenyatta kuonesha ushirikiano wa dhati na Mahakama
ya Kimataifa, kwani Kenya ina mchango mkubwa katika mchakato dhidi ya vitendo vya
kigaidi Barani Afrika.