2013-10-18 08:11:29

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 29 ya Mwaka C wa Kanisa


Ewe mpendwa msikilizaji wa Neno la Mungu, tunasonga mbele katika kipindi chetu, kawaida tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu. Tayari tuko karibu ng’ambo ya pili katika mwaka wa Kanisa yaani Dominika ya 29 ya mwaka C. RealAudioMP3

Mama Kanisa atuwekea Neno lenye kutuhimiza kusali bila kuchoka, ndiyo kusema, kusali kwa matumaini daima. Twaweza kuanza tafanario yetu kwa kujiuliza maswali kadhaa ya msingi: Kwa nini tunasali?, Namna gani tusali? Na ni kitu gani cha kuomba toka kwa Mungu?

Mpendwa mwana wa Mungu, jambo la kusali ni jambo gumu na nyeti, lakini basi Injili ya leo, mwongozo wa maisha yetu yaweza kutusaidia kuweza kujibu maswali haya! Tukianza na mfano alioutoa Bwana tunakutana na watu watatu wakiwa ni hakimu, mjane na yule mdhulumu wa mjane huyu. Mama mjane aliye kiini cha simulizi la Injili anawakilisha upande wa maskini, waliosukumizwa pembezoni yaani wasiofikirika kuwa waweza kutoa mchango wowote katika jamii yao. Mama huyu anajikuta mbele ya mdhulumu wake ambaye hataki kutambua haki yake.

Kwa upande mwingine mama mjane anajikuta mbele ya hakimu ambaye badala ya kushughulikia haki katika jumuiya, yuko katika kujisikia kama mtu asiyehitaji kusumbuliwa. Injili haioneshi ugumu wake unatokea wapi lakini twaweza kusema ni katika kumezwa na mamlaka ya kidunia! Ukaidi wa hakimu unajionesha katika mfano kwa maneno ya Bwana “ alikuwa hamwogopi Mungu na wala hakumjali mtu awaye yote” Hii yamaanisha tendo la kujisalimisha kwa shetani na hivi kuyakimbia maongozi ya Mungu katika maisha yako.

Tendo la kutowajali wengine lataka kutuambia tabia ya moyo wa hakimu yaani, hauko tena katika kutazama mafaa ya wengine bali mafaa binafsi. Amejifungia katika kovu lake na hivi hakuna aina yoyote ya sala inayopenya kovu hilo! Ni ajabu mwanadamu wee, kugangamala kiasi hicho! Hebu legeza moyo ukaguswe na fadhili za Mungu!

Mpendwa msikilizaji, mama mjane yuko katikati ya hali ngumu ambayo utatuzi wake pengine hauonekani! Lakini Bwana anakuja na njia mwafaka, njia ya Kimungu, hapa ndipo panazaliwa sala! Sala hii ni rufaa, ni kilio, ni kunyanyua mikono kuelekea mbinguni, kama alivofanya Musa katika somo la kwanza akisali kwa ajili ya kuomba msaada wa Mungu ili Waisraeli wapate ushindi dhidi ya Waamaleki. Pengine sala hii inaweza ikawa ni ya kutafuta masilahi binafsi lakini si hivyo! Yatupasa kusali hata wakati wa taabu, chamsingi ni kutambua wajibu wetu daima wa kusali na kutekeleza yote ambayo Mungu anataka tufanye.

Mtakatifu Inyasi wa Loyola anasema, salini kana kwamba matokeo yote ya sala yanakutegemea wewe mwenyewe, na wakati huohuo salini na jiweke chini ya Bwana kana kwamba matokeo yote ya sala yanamtegemea Mungu. Kwa hakika mpendwa msikilizaji kuna nafasi ya uwajibikaji kama Musa na Yoshua walivyokuwa wakiwajibika na hivi Mungu anakamilisha sala yao. Ndiyo kusema huyu mama mjane amefanya vema kuwajbika ili kulinda haki yake na haki ya kijumuiya.

Baada ya kuwajibika basi, ugumu waweza kujitokeza na kwa namna hii sala inazaliwa ili kusafisha na kulainisha yale ambayo yaonekana kuwa magumu. Sala inakuwa si tu mwafaka bali pia ya lazima. Kama ndivyo basi, inatulazimu kugundua sala iwe ya namna gani? Namna gani twaweza kusali na kusonga mbele bila kuanguka na kukata tamaa?

Ndiyo kusema inaweza kutokea hatuoni matokeo na hivi tukaanza kujiuliza Mungu yuko wapi, mbona haingilii kati katika tatizo langu au katika tatizo hili? Katika hili daima maadhimsho yetu ya kilitrujia hutupa jibu na jibu ni Imani. Imani huamini bila kuona, bila kujali faida ya kidunia bali uzima wa milele, imani humsukuma mtu abaki katika sala iliyo mnyororo, sala ya kudumu kama Injili inavyotufundisha.

Mwaka huu ni mwaka wa imani, kumbe ni lazima kurudi nyuma na kuthibitisha imani yetu na njia mojawapo ni kuiishi kwa njia ya sala, sala isiyochoka kama sala ya mama mjane katika Injili tunayoitafakari. Kama basi sala yetu itafanya daima marejeo katika imani, ni kwa hakika haitachoka na kinyume chake ni sahihi pia! Imani hutufundisha mwendelezo wa maisha toka uumbaji hadi mwisho wa nyakati tofauti na kusadiki katika mabadiliko mbalimbali katika dunia ya sasa na itikadi mbalimbali ambazo nyingine hutaka kuondoa maisha na uhai wa watu.

Barua ya kitume Mwanga wa Imani yatualika kutafakari juu ya uhusiano uliopo kati ya imani na vielelezo vyake yaani sakramenti na hasa ubatizo, kipaimara na Ekaristi Takatifu. Ni katika sakramenti hizi mtu mwamini hugundua kina mtima wa mapendo ya Mwenyezi Mungu kwa mwanadamu. Jambo hili hatuwezi kulifikia pasipo maisha ya sala iliyo njia ya mawasiliano na Mungu.

Mpendwa msikilizaji, katika maisha ya imani lazima kuongeza kitu kingine kama asemavyo Yakobo Mtume, matendo ya mapendo. Katika somo la kwanza tunaona pamoja na imani lazima Musa ainue mikono juu wakati huohuo akimwomba Mungu. Katika maisha ya imani lazima kulia kwa kilio kitokacho katika mtima wangu, kama mjane anavyofanya mbele ya hakimu, kama tuliavyo tunapoimba au kusali kimya zaburi ya 130, tukisema Bwana kama wewe ungalihesabu maovu yetu nani angesimama?

Mpendwa mtoto anapozaliwa jambo la kwanza ni kutoa kilio kama hakikisho la haki yake ya kuishi na hivi tunaweza kufananisha kilio cha mtoto mchanga na kilio chako mwamini kwa ajili ya imani, kwa ajili ya mapendo na mshikamano katika maisha ya watu. Kilio ambacho chajenga uhusiano na Mungu kwa njia ya sala.

Mpendwa msikilizaji katika maisha ya imani yaweza kutokea kuchoka, na hivi tukate tamaa au tufanyeje! Mungu hatuachi bila majibu na suluhisho la jambo hilo. Tunamwona Musa anapoinua mikono peke yake anachoka na hivi anapata msaada wa Aroni.

Kumbe, shida tulizonazo tunaweza kuzishinda tukijiaminisha katika maisha ya pamoja ndiyo kusema maisha ya Jumuiya. Kama mikono inachoka basi pembeni kuna mwingine anayetupa msaada ili uweze kufika mwisho, ndiyo maana ya uwepo wa mapadre wa kiroho katika maisha yetu ya Kikristo. Hapa tunapata jibu la swali la Bwana, je Mwana wa mtu ajapo atakuta imani duniani? Kwa hakika ataikuta! Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.