Shikamaneni, tafuteni mafao ya wengi, changamoto za sasa ni mapito ya mchakato wa
Katiba mpya!
Dr. Adelardus Kilangi, Mwenyekiti wa Tume ya Sheria za Kimataifa, Umoja wa Afrika
katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha kwamba, mchakato wa Katiba ya
Tanzania ni fursa ya pekee kwa watanzania katika historia kuweza kushiriki moja kwa
moja katika kutunga Katiba ya nchi ambayo kimsingi ni sheria mama. Katiba zote zilizotangulia
zilitungwa na makundi ya watu kwa niaba ya watanzania wengine.
Kwa maoni
yake anasema, mchakato wa Katiba unaendelea vyema na kwamba, tayari Rasimu ya Katiba
Mpya imekwisha kupatikana na Bunge maalum la Katiba litaundwa hivi karibuni ili kupitisha
au kuukataa Mswada wa Katiba Mpya ya Tanzania na hatua itakayofuata ni kurudisha Muswada
huo kwa wananchi ili waweze kuupigia kura ya maoni.
Dr. Kilangi anasema, mchakato
huu unaendelea kukabiliwa na changamoto nyingi hasa zaidi ni: kukosekana kwa msimamo
wa pamoja kuhusu suala la Muungano, Serikali katika muungano na mawazo baadhi ya watu
kwamba, mchakato umetekwa na Chama cha Mapinduzi. Ikumbukwe kwamba, hizi ni changamoto
za kawaida katika mchakato wa kutunga Katiba ya Nchi yoyote ile.
Dr. Kilangi
anasema, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, watanzania wanaendelea kushikamana
kwa dhati, daima wakitafuta hatima yao kama watanzania; wadau mbali mbali washiriki
katika mchakato kwa ajili ya mafao ya wengi na wala si kwa ajili ya kikundi fulani
cha watu ndani ya Jamii ya Watanzania. Watanzania wakizingatia ushauri huu, watafanikiwa
kupata Katiba mpya hata kama kwa sasa inaonekana kwamba, kuna changamoto nyingi!