Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema kuna haja ya taasisi za mafunzo ya uongozi
za China na Tanzania kuandaa kozi zenye kuwafaa makundi fulani ya viongozi ambazo
zitasaidia kubadili mwelekeo wao na utendaji wao wa kazi hasa katika masuala yanayohusu
sekta binafsi.
Amesema taasisi hizo zinapaswa kuwa na uelewa mkubwa kuhusu
ushirikiano wa pamoja baina ya sekta binafsi na za umma (PPP), zinapaswa kujua faida
za ushirikiano huo na zinapaswa kubainisha ni sekta zipi zinapaswa kutekeleza mpango
huo wa ushirikiano.
Ametoa kauli hiyo Ijumaa, Oktoba 18, 2013 wakati akifungua
mafunzo ya siku 14 kwa maafisa 20 kutoka idara na taasisi za serikali ya Tanzania
yanayoendeshwa kwa pamoja baina ya Chuo cha Uongozi cha China na Taasisi ya Uongozi
ya Tanzania.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mpango wa Serikali kuboresha utendaji
wa Maeneo ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZ) yameanza leo kwenye Chuo cha Uongozi
cha China (China Governance Academy), jijini Beijing, China.
Alisema Tanzania
imefanya maamuzi ya kutumia ushirikiano wa pamoja baina ya sekta binafsi na za umma
(PPP) kama njia ya kukuza na kuendeleza miundombinu, kuhamisha ujuzi na teknolojia
pamoja na ujenzi wa viwanda.
“Ni muhimu taasisi zetu hizi mbili zikatambua
jambo hili na kuchangia kwa juhudi zote ili kuhakikisha kuwa linafanikiwa,” alisema.
Alisema kozi kama hizo zinapaswa kuwalenga watumishi kutoka taasisi za serikali
pamoja na sekta binafsi na akazitaka taasisi hizo kuhakikisha zinaisaidia kuwepo kwa
ufanisi wa hali ya juu kwenye ushirikiano wa pamoja baina ya sekta binafsi na za umma.
“Muwasaidie watu hawa waweze kutambua ni wakati gani ushirikiano wa aina hii unakuwa
wa manufaa zaidi kwa wahusika, ni wakati gani wahusika wanafaidika na PPP, je wanakabiliwa
na changamoto zipi, na wanafanyaje ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza,”
aliongeza.
Alisema jambo lililo wazi kuwa ushirkiano baina ya wajasiriamali
wa Kichina na wa Kitanzania utasaidia kuongeza fursa za kuhamisha ujuzi na teknolojia
pamoja na kuendeleza miundombinu. “Natambua kwamba kuna wafanyabiashara zaidi ya 500
wa kutoka China ambao wako nchini Tanzania, hawa wanachangia maendeleo ya kiuchumi
Tanzania kwa kuingiza teknolojia mpya na kutoa fursa za ajira,” aliongeza.
Waziri
Mkuu ambaye yuko katika siku ya tatu ya ziara ya kikazi yake ya siku tisa kwa mwaliko
wa Serikali ya nchi hiyo, alitembelea kiwanda cha aluminium cha China CHINALCO) na
kiwanda cha kutengeneza zana za kijeshi ambako alionyeshwa bidhaa mbalimbali zinazozalishwa
na viwanda hivyo.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu amefuatana na Waziri wa Nchi,
(OWM) Uwezeshaji na Uwekezaji, Dk. Mary Nagu; Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah
Kigoda; Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe; Waziri wa Uvuvi na Mifugo wa Zanzibar,
Bw. Abdallah Jihad Hassan; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bw. Mahadhi Juma Maalim na Naibu Waziri wa Fedha, Bibi Saada Salum Mkuya.
Pia
amefuatana na Balozi wa China, Luteni Jenerali (Mst.) Abdulrahaman Shimbo, Wakuu wa
mikoa ya Mtwara, Shinyanga na Simiyu; wabunge wawili, Bw. Godfrey Zambi (Mbozi) na
Dk. Titus Kamani (Busega) na viongozi wakuu wa Tanzania Private Sector Foundation,
Bw. Reginald Mengi, Bw. Salum Shamte na Bw. Godfery Simbeye.