Yanayoendelea kujiri katika ziara ya Waziri Mkuu Pinda nchini China!
Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amewasili Beijing, China siku ya Jumatano, Oktoba
16, 2013 na kuanza vikao ikiwa ni sehemu ya ziara ya kikazi ya siku tisa kwa mwaliko
wa Serikali ya nchi hiyo.
Mara baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa
Beijing, Waziri Mkuu alielekea kwenye nyumba ya wageni ya Serikali ya Diaoyatui ambako
alipokea taarifa fupi kuhusu hali ya kisiasa na kiuchumi nchini China.
Akiwasilisha
taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Balozi wa Tanzania nchini China, Luteni Jenerali
(Mst.), Abdulrahman Shimbo alisema sehemu kubwa ya utekelezaji wa miradi kati ya Tanzania
na China iko chini ya mwamvuli wa FOCAC (Forum on Africa China Cooperation) ambayo
inagawanyika katika maeneo sita.
Alyataja maeneo hayo kuwa ni misaada (grants),
mikopo ya masharti nafuu (preferential loans), mikopo ya kibiashara (preferential
buyers credit), uwekezaji, ushirikiano maalum na ushirkianao wa kihistoria.
“Miradi
mahsusi inayogharimiwa kwa pamoja baina ya Serikali ya Tanzania na China imeongezeka
sana na inatarajiwa kufikia Dola za Marekani milioni 800 ifikapo mwaka 2014/2015,”
alisema Balozi Shimbo.
Kuhusu elimu na mafunzo, Balozi Shimbo alisema programu
hiyo ambayo imeanza muda mrefu, hadi kufikia Desemba 2011, ilikuwa imekwishawanufaisha
wanafunzi wa Kitanzania 110 na wataalamu 1,020 ambao walipatiwa mafunzo chini ya udhamini
wa Serikali ya China.
Kwa mwaka huu 2013, Balozi Shimbo alisema kuna wanafunzi
zaidi ya 300 ambao wanasoma nchini humo. “Hivi sasa kuna wanafunzi 31 wanaodhamimiwa
na serikali ya Tanzania, wanafunzi 249 wanaofadhiliwa na serikali ya China na wengine
zaidi ya 100 wanaojidhamini wenyewe katika shahada za Uzamili na Uzamivu,” alisema.
Pia alisema Tanzania kwa kushirikiana na Dalian University of China, itanufaika
na mradi wa kupandisha hadhi Chuo cha Usafiri wa Baharini (Dar es Salaam Maritime
Institute) hadi kufikia ngazi ya Chuo Kikuu cha Kanda ya Afrika Mashariki.
Alisema
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekabidhi kwa kampuni ya Kichina ya China Rail
Engineering Group ambayo inakifufua kiwanda cha viatu na ngozi cha Zanzibar na kukifanya
kiwe kiwanda cha samani. Kiwanda hicho kilijengwa kwa msaada wa Serikali ya China
katika miaka ya 70.
Hata hivyo, Balozi Shimbo alisema Tanzania inakabiliwa
na changamoto kubwa ya kimahusiano na China ambapo vijana wa Kitanzania 175 wapo katika
magereza ya nchini China kutokana na makosa ya uhalifu yakiwemo ya kusafirisha madawa
ya kulevya.
“Kati ya hao, watatu uraia wao ni wa kutiliwa mashaka. Kati yao
48 wako China Bara, Hong Kong wapo 117 na Macao wapo 10. Kati ya hao 175, wanawake
ni 34, ambapo 28 wako Hong Kong na sita wako China bara,” alisema.
Akizungumza
na maafisa ubalozi pamoja na wajumbe wa msafara wake, Waziri Mkuu alisema tatizo la
madawa ya kulevya linaharibu sifa ya Tanzania pamoja na mahusiano baina yake na nchi
marafiki.
“Tunahitaji kufanya kazi ya ziada ili kupambana na wasafirishaji
wa dawa za kulevya. Watu 175 ni wengi kwa nchi moja lakini cha kusikitisha zaidi ni
idadi kubwa ya wanawake waliokamatwa... wizara zinazohusika inabidi tukae na kuweka
mkakati wa pamoja,” alisema.
Kuhusu misaada ya China kwa Tanzania, Waziri Mkuu
alisema, kuna miradi ya kufa na kupona ambayo itabidi iwekewe uzito katika ziara yake
hii na kuiainisha kuwa ni ujenzi wa reli ya kati, usambazaji wa umeme na ukuzaji wa
utalii baina ya Tanzania na China hasa fursa ya kuanzisha usafiri wa ndege wa moja
kwa moja baina ya Chiona na Tanzania.
Alhamisi, Oktoba 17, 2013 Waziri Mkuu
anafanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Mhe. Li Keqiang, Rais wa Benki ya
Exim ya China, Rais wa Benki ya Maendeleo ya China na uongozi wa China Railway Jianchang
Engineering.