Simameni kidete kulinda na kutetea masilahi ya wengi, haki na amani!
Viongozi wa Serikali nchini Tanzania wametakiwa kutotafuta masilahi yao binafsi kwa
kupitia migogoro mbalimbali inayojitokeza kati ya wafugaji na wakulima, bali wanatakiwa
kutafuta ufumbuzi na kumaliza migogoro ya kijamii ili amani na utulivu viendelee kutawala.
Kauli
hiyo imetolewa Siku ya Jumatano na Imamu Hilali Abdula Azizi Yunus wa msikiti wa Bilali
area C Dodoma alipokuwa akihutubia baada ya swala ya Eid-El-Hajj iliyofanyika viwanja
vya Barafu mjini hapa.
Imamu huyo alisema kuwepo kwa migogoro hiyo siyo wakati
wa kujitafutia masilahi, bali kinachotakiwa ni upatikanaji na ufumbuzi wa namna amani
itakayotakiwa ipatikane kati ya pande zote mbili. Alisema kitendo cha kuendelea vurugu
na serikali kukaa kimiya hali hiyo inatia wasiwasi kwa watanzania na kushuku kuwa
pengine viongozi hao wa serikali wanapata masilahi kwa kupitia migogoro hiyo.
Alisema
Serikali ina wajibu wa kutatua migogoro inayojitokeza nchini Tanzania kutokana na
uwezo na nguvu iliyopo, hivyo hakuna sababu ya kusikia wananchi wanapigana na kuuwana
kwa ajili ya malisho ya mifugo na maeneo ya kilimo. Watanzania hawaamini kwamba, serikali
kama inaweza kushindwa kama ule mgogoro uliopo kati ya wafugaji na wakulima wilayani
Mvomero ambao umekuwa ukichukuwa sura mpya kila unapotokea kwa muda mrefu sasa.
“Hivi
kweli serikali ilivyo na nguvu imeshindwa kutatua hii migogoro ya wafugaji na wakulima
ikiwemo ile ya wananchi pia kuchomewa nyumba zao na wengine kudaiwa kubakwa, hapa
kuna maslahi ndani yake” alisema Imamu.
Wakati huo huo Shekhe wa Mkoa wa Dodoma
Rajabu Shabani akihutubia baada ya swala hiyo kwenye msikiti wa Gadaff, amewataka
viongozi wa kiasiasa nchini Tanzania kuacha kupeleka hisia zao kuhusu suala la marekebisho
ya katiba mpya na badala yake wazingatie maoni ya Watanzania ambao walipelekewa kwa
ajili ya kutoa mapendekezo ya namna wanavyotaka rasimu ya Katiba iwe.
Shekhe
huyo alisema hata hivyo anategemea viongozi wa vyama vya siasa ambao wamekutana na
Rais Jakaya Kikwete mapema Juma hili pia watafanya yale ambayo yatakuwa yana maslahi
kwa Watanzania wote na siyo kwa upande wao na vyama vyao!