Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inaboresha mfumo wa chakula
ili kupambana kufa na kupona na baa la njaa na utapiamlo duniani. Hiki ndicho kiini
cha maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani ambayo kwa Mwaka 2013 yanaongozwa na kauli
mbiu "watu wenye afya wanategemea mfumo bora wa chakula". Maadhimisho haya kwa namna
ya pekee yamefanyika kwenye Makao Makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa
Mataifa, FAO yaliyoko mjini Roma.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake
kwa Maadhimisho haya uliosomwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Luigi Travaglino anasema,
ni kashfa kwa dunia kuendelea kuwa na watu wanaoteseka kutokana na baa la njaa na
utapiamlo. Maadhimisho haya yamefanyika kwenye nchi 150, wanachama wa FAO, kama sehemu
ya kumbu kumbu ya kuanzishwa kwa FAO, hapo tarehe 16 Oktoba 1945. Maadhimisho haya
yamefanyika wakati kuna watu millioni 842 wanaobaliwa na baa la njaa na utapiamlo.
Baa
la njaa anasema Baba Mtakatifu Francisko ni matokeo ya ubinafsi, falsafa ya kutowajali
wengine, kiasi cha kuona kwamba, baa la njaa ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu.
Baa la njaa na utapiamlo ni majanga yanayomwandama mwanadamu na wala si sehemu ya
mfumo wa maisha yake. Kutokana na changamoto hii kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa
kuhakikisha kwamba, inafanya mabadiliko sanjari na kuboresha mfumo wa chakula kwa
kukazia pia mshikamano na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Jumuiya ya Kimataifa anasema Baba Mtakatifu haina budi kujenga utamaduni wa
mshikamano pamoja na kuhakikisha kwamba, watu wanakuwa na matumizi bora ya chakula,
kwani kuna kiasi kikubwa cha chakula kinachotupwa kila siku, wakati ambapo kuna watu
wanateseka kwa baa la njaa na utapiamlo.
Kwa upande wake Bwana Josè Graziano
da Silva, Mkurugenzi mkuu wa FAO, katika maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani anasema,
uhakika wa usalama wa chakula unaweza kufikiwa, ikiwa kama kuna mfumo makini wa chakula
unaoweza kuzalisha chakula kinachotosheleza mahitaji ya wengi. Hali ya chakula inaonesha
kwamba, kuna watu wachache wanaokula na kusaza wakati ambapo kuna kundi kubwa la watu
wanaoogelea katika baa la njaa na utapiamlo.
Gharama za baa la njaa zinatisha
kwani, dunia inapoteza kiasi cha asilimia tano ya nguvu ya uzalishaji mali duniani,
hali inayochangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la huduma za afya. Dunia inaweza kufaidika
kiuchumi, ikiwa kama baa la njaa na utapiamlo litaweza kudhibitiwa kikamilifu. Kati
ya nchi 128, ni nchi 62 tu ndizo ambazo zimefanikiwa kufikia lengo la Maendeleo ya
Millenia kwa kufuta baa la njaa na utapiamlo, hali inayoonesha kwamba, ushindi dhidi
ya baa la njaa ni jambo linalowezekana, ikiwa kila mdau atatekeleza dhamana na wajibu
wake.
FAO inasema kwamba, Siku ya Chakula Duniani ni fursa kwa Jumuiya ya Kimataifa
kufanya upembuzi yakinifu ili kubainisha tiba itakayoganga baa la njaa na utapiamlo
duniani na kwamba, majanga haya ni matokeo ya mfumo mbovu wa chakula.
Akichangia
mada kwenye Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani, Mama Nadine Heredia, mke wa Rais
wa Perù, amewataka wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanatoa dira na mwongozo
utakaosaidia kupambana na baa la njaa na utapiamlo sanjari na kuzingatia: afya, elimu
na usawa wa kijinsia, kwa kuwekeza zaidi kwa wanawake kwani hawa ni wadau wakubwa
katika mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo.
Anasema, Jumuiya ya Kimataifa
inahitaji sera makini za kiuchumi zitakazosaidia ukuaji wa uchumi na maboresho ya
maisha ya kijamii, mambo yanayochangiwa kwa kiasi kikubwa na uwekezaji katika huduma
makini za kijamii. Ukuaji wa uchumi hauna budi kuleta faida kwa wananchi wengi zaidi:
kwa wale wanaoishi vijijini na mijini; wanawake kwa wanaume.
Wakati huo huo,
Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, inatoa chakula kwa watu wanaokufa
kwa njaa pamoja na kuweka mikakati ya muda mfupi na mrefu katika mapambano dhidi ya
njaa na utapiamlo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Naye Kanayo
Nwanze, Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Kuendeleza kilimo na chakula, IFAD anasema,
wakulima wadogo wadogo wanachangia kwa kiasi kikubwa katika maboresho ya mfumo wa
chakula, ikiwa kama watabahatika kuwa na miundo mbinu bora, siasa safi, elimu, ujuzi
na maarifa. Haya ni mambo ambayo yamejionesha nchini Brazil, Cina, Malasiya na Vietnam,
kiasi kwamba baa la njaa kwa sasa limepewa kisogo.
Anasema, IFAD itaendelea
kushirikiana na Serikali mbali mbali duniani, ili kuhakikisha kwamba, zinaibua sera
na mikakati makini, ili kuwekeza katika miundo kwa nia ya kupambana na baa la njaa
duniani.
Wanawake wana mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya baa la njaa
na utapiamlo. Ni mchango kutoka kwa Ertharin Cousin, Mkurugenzi mtendaji wa Mfuko
wa Maendeleo ya Kilimo wa Umoja wa Mataifa. Anasema, mikakati mingi vijijini, bado
inaendelea kuwabagua wanawake, hili ni jambo ambalo halina budi kusitishwa mara moja
ili kuleta ufanisi katika maboresho ya mfumo wa chakula duniani. Wanawake wakiwezeshwa,
watachangia kwa kiasi kikubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa kuweza kufikia malengo yake
ya kupambana kufa na kupona na baa la njaa na utapiamlo duniani.
Mchakato huu
hauna budi kuungwa mkono na mabadiliko ya tamaduni kwa kutambua kwamba, chakula ni
haki msingi ya binadamu na kwamba, kila mtu anayo haki ya kuwa na uhakika wa chakula.
Jambo hili linawezekana ikiwa kama watu watabadilisha tabia na utamaduni wa kutupa
chakula wakati kuna mamillioni ya watu wanakufa kwa njaa na utapiamlo. Ni mchango
wa Bwana Nunzia De Girolamo, Waziri wa Sera ya kilimo, chakula na misitu wa Italia,
wakati akichangia mada katika Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kwa Mwaka 2013,
mjini Roma.