Msumbiji yaukumbuka wema na ukarimu wa Baba wa Taifa Mwalimu J. K. Nyerere!
Wananchi wa Msumbiji na Wanatanzania wanaoishi nchini Msumbiji kwa pamoja, jumapili
iliyopita waliungana katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumbu kumbu ya miaka
14 tangu alipofariki dunia mtumishi wa Mungu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye
mchakato wa kumtangaza kuwa Mwenyeheri unaendelea Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania.
Mwalimu Nyerere alikuwa ni mtu mwenye imani kuu na mwanasiasa mahiri na kila
jambo alilipatia nafasi yake na kamwe hakuchanganya mambo. Ni kiongozi aliyepigania
haki msingi za binadamu, akakazia uhuru, umoja, upendo na mshikamano kati ya watu.
Alikuwa ni mtu wa shukrani aliyetambua nafasi ya Mungu katika maisha yake kama mwamini
na mwanasiasa. Daima alimtanguliza Mwenyezi Mungu katika mipango na mikakati yake
ya maisha. Ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Padre Joseph Juma, OFM wakati wa
kumbu kumbu ya miaka 14 tangu alipofariki dunia Mwalim Nyerere.
Mwalimu anakumbukwa
na wengi kwa kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi, demokrasia na uhuru
wa kweli. Ni kiongozi aliyekuwa na upeo mkubwa katika maisha. Ataendelea kukumbukwa
na wengi, wakati huu watu wanapoanza kukengeuka kutokana na udini, ukabila, rushwa
na ufisadi wa mali ya umma.
Katika tukio hili ambalo limewagusa wananchi wengi
wa Msumbiji wanaokumbuka fadhila na ukarimu wa Mwalimu Nyerere kwa watu waliokuwa
wanateseka kutokana na ukoloni. Rais mstaafu Joaquim Chisano wa Msumbiji, amemshukuru
Mwalimu kwa mchango wake mkubwa katika harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika. Ni
kiongozi aliyetambua na kuthamini mchango wa wapigania ukombozi nchini Msumbiji, akajitosa
kimasomaso kuwasaidia kwa hali na mali.
Wakati wa mapambano ya vita vya wenyewe
kwa wenyewe nchini Msumbiji, wananchi wengi waliogopa kwenda kusali Makanisani au
misikitini, lakini Mwalimu Nyerere kila wakati alipokuwa anafika nchini Msumbiji,
hakukosa kwenda kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa la Mtakatifu
Antonio da Polana.
Ni mwamini na kiongozi aliyeonesha unyenyekevu wa hali
ya juu, akawapenda na kupendwa na watu kutoka ndani na nje ya Tanzania. Kwa hakika
Mwalimu alikuwa ni mtu wa watu na kamwe hakupenda makuu, kwani kwa wanyonge alikuwa
mnyonge ili aweze kuwaonjesha upendo wa kibaba.
Rais mstaafu Chisano anasema
kwamba, Mwalimu alipong'atuka kutoka madarakani na baadaye kupata nafasi ya kutembelea
tena Msumbiji, Rais Chisano wakati huo, aliamua kumtembeza Mwalimu mjini Msumbiji,
ili aweze kujionea hali halisi ya maisha ya watu wa Msumbiji. Alimshauri kuwekeza
kwa wafanyabiashara wadogo wadogo waliokuwa wanauza bidhaa barabarani, ili hatimaye,
waweze pia kuchangia katika kuinua uchumi na pato la taifa badala ya kujenga tabia
ya kuwa omba omba na wategemezi.
Rais mstaafu Chisano anasema, maneno haya
kutoka kwa Mwalimu yameendelea kuwa ni changamoto kubwa katika maisha yake kama Rais
na raia wa Msumbiji. Anasema, ili taifa liweze kusonga mbele linahitaji: watu, ardhi,
siasa safi na uongozi bora, tunu msingi ambazo zilisimamiwa kwa dhati na Mwalimu Nyerere
wakati wa uhai wake, changamoto hata kwa viongozi wengine Barani Afrika.
Naye
Dr. Shamin Nyanduga, Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji anasema kwamba, Mwalimu Nyerere
alikuwa ni kiongozi mwaminifu kwa Serikali na dini yake ndiyo maana Jimbo Katoliki
la Musoma limeanzisha mchakato wa kutaka atangazwe kuwa Mwenyeheri na hatimaye mtakatifu,
kama mfano wa kuigwa na waamini walei.
Ni kiongozi aliyejitahidi kutumia vipaji
na karama zake kwa ajili ya mafao ya wengi. Alihamasisha matumizi sahihi ya rasilimali
ya taifa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wote. Ni kiongozi aliyetegemewa na wengi
kwa ushauri kutokana na hekima na busara ambayo alikirimiwa na Mwenyezi Mungu.