2013-10-16 08:15:03

Jengeni utamaduni wa kusoma kwa bidii, juhudi na maarifa sanjari na kudumisha nidhamu!


Mheshimiwa Padre Pius Mgeni, Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania, SAUT amewataka wanafunzi wa Chuo Kikuu cha SAUT kujenga na kudumisha moyo wa kusoma kwa bidii, juhudi na maarifa, daima wakijitahidi kutumia vyema rasilimali muda iliyoko mbele yao, kwani kishawishi kikubwa kwa wanafunzi wengi ni kujidanganya kwa kudhani kwamba, muda bado! RealAudioMP3

Ameewataka wanafunzi wa SAUT kujenga utamaduni wa kujipatia ujuzi na maarifa kwa kuwa na matumizi makini ya Maktaba ya Chuo ambayo inaendelea kuboreshwa zaidi ili kukidhi mahitaji na viwango vya elimu ya juu kitaifa na kimataifa.

Padre Pius Mgeni ameyasema hayo hivi karibuni wakati wa ufunguzi wa Mwaka wa Masomo SAUT kwa mwaka 2013- 2014. Amekazia umuhimu wa kujenga uhusiano mwema na wenye tija na waadhili wa Chuo Kikuu cha SAUT kwa kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema muda uliopangwa kwa ajili ya mashauri. Padre Mgeni amesikitika kuona kwamba, kuna idadi kubwa ya wanafunzi ambao wameanza kujenga tabia ya kurudia mitihani, kiasi kwamba baadhi ya wanafunzi wameanza kupewa “viti maalum” au kushirikishwa kwenye “Bunge maalum”, lugha inayotumika kwa wanafunzi wanaorudia mitihani mara kwa mara!

Padre Pius Mgeni ambaye ameteuliwa hivi karibuni na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuwa Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha SAUT na hivyo kuchukua nafasi ya Dr. Charles Kitima aliyehitimisha muda wake wa uongozi Chuoni hapo, amewataka wanachuo kutumia uhuru wao kwa kuwajibika zaidi na zaidi, kwa kutambua kwamba, uhuru unaowajibisha ni kati ya tunu msingi ambazo mwanadamu amekirimiwa na Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha yake hapa duniani.

Amewataka wanafunzi kujijengea mazingira ya kuelimika na kujielimisha na Jamii iwatambue kutokana na matumizi sahihi ya elimu yao. Chuo kikuu kisiwe ni mahali pa kuporomoka kwa maadili na utu wema kwa kujiingiza katika mambo ambayo ni kinyume cha maadili.

Padre Mgeni amewataka wanafunzi kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema akili, utashi, nidhamu na tabia njema kama kielelezo cha ufanisi katika mchakato wa elimu; wawe kweli ni wasomi walioelimika. Amekemea tabia ya baadhi ya wanafunzi kuanza kujiingiza katika masuala ya matumizi haramu ya dawa za kulevya, unywaji wa kupindukia pamoja na biashara ya ngono, mambo ambayo kimsingi ni kielelezo cha kumong’onyoka kwa maadili na utu wema.

Amewataka wanafunzi wa SAUT kutumia hekima na busara katika safari ya maisha yao hapo Chuoni. Waheshimu na kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya Chuo Kikuu cha SAUT, Kanisa na Jamii ya watanzania katika ujumla wake.

Padre Pius Mgeni amewashukuru na kuwapongeza wakuu wa vitivo mbali mbali vya SAUT kwa ujasiri, majitoleo na kazi nzuri wanayoendelea kuifanya kwa ajili ya maboresho ya elimu ya juu nchini Tanzania na Afrika Mashariki katika ujumla wake. Kwa tukio hili la ufunguzi wa Mwaka wa Masomo, Chuo Kikuu cha SAUT, Mheshimiwa Dr. Pius Mgeni alikuwa anaanza rasmi utume wake kama Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania.

Kutoka SAUT, Mwanza, Tanzania ni
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.