2013-10-16 11:06:34

Chama cha Msalaba Mwekundu Kenya, kugharimia huduma za matibabu kwa waathirika wa shambulio la kigaidi Kenya!


Bwana Abbas Gullet, Katibu mkuu wa Chama cha Msalaba Mwekundu nchini Kenya amesema kwamba, chama chake kitalipa kiasi cha shilingi za Kenya millioni 47 kwa ajili ya gharama za matibabu kwa watu waliokumbwa na mkasa wa shambulizi la kigaidi la Westegate, lililotokea hivi karibuni nchini Kenya.

Hadi kufikia tarehe 14 Oktoba 2013, kiasi cha shilingi za Kenya millioni 123 zilikuwa zimekwisha kusanywa tayari kutoka kwa wananchi na watu wenye mapenzi mema. Kiasi cha shilingi millioni 47 kitatolewa kwa Hospitali ambazo zimetoa huduma kwa waathirika wa shambulizi hilo la kigaidi nchini Kenya.

Kiasi cha shilingi millioni 15 kitatolewa kwa waathirika wenyewe. Chama cha Msalaba Mwekundu kimeyataka pia Makampuni ya Bima kugharimia huduma za matibabu kwa wateja wao kadiri ya sheria za nchi.

Katika shambulio lililotokea nchini Kenya hapo tarehe 21 Septemba, 2013, watu 67 walifariki dunia, wengine 240 kujeruhiwa vibada na watu wengine 23 hawajulikani waliko. Bado kuna wagonjwa 10 ambao wanaendelea kupata tiba nchini Kenya.







All the contents on this site are copyrighted ©.