2013-10-15 08:12:04

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 28 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa


Mpendwa msikilizaji, ninapenda kukusalimu na kukualika katika kipindi cha tafakari ya Neno la Mungu : masomo Dominika 28 ya mwaka C. Neno la Mungu latudai kuwa wenye imani inayorudisha upendo na shukrani kwa Mwenyezi Mungu.

Katika somo la kwanza tunamwona Naamani, jemedari mpagani mara baada ya kuponywa ukoma wake anarudisha tunda la shukrani kwa Mungu kwa njia ya mtumishi wa Mungu. Naamani ni mfano bora katika upagani wake wa kutoa shukrani kwa Mungu.

Basi wale wote waliowabatizwa wanadaiwa zaidi kuliko mpagani huyu Naamani katika wajibu wa kumrudishia Mungu shukrani kwa ajili ya ukombozi walioupokea kwa njia ya Damu Azizi ya Bwana pale msalabani. Katika somo la II Mt. Paulo anamwasa Mtakatifu Timotheo, daima kuweka mawazo na kumbukumbu zake zote katika Yesu Kristu mfufuka.

Akimwambia hilo anasema si wewe tu, bali hata yeye mwenyewe ni mteswa wa Bwana na zaidi katika utume wake. Katika hilo anasema Neno la Mungu ni hai halifungwi katika mateso hayo bali tunazidi kulichangamkia ili liweze kupiga mbio na kufikia lengo lake la kuwaokoa watu. Anamkumbusha Mtakatifu Timotheo ukuu wa Mungu akisema, hata sisi tusipoamini, upendo na uaminifu wa Mungu hubaki palepale! Kumbe sasa mwaliko ni kustahimili katika mausia na mafundisho yake Mungu ili kuweza kubaki naye daima, tukitumikia sas ana kisha kuurithi uzima wa milele.

Mpendwa msikilizaji, Injili yaweka mbele yetu, Bwana wetu Yesu Kristo aliyeko katika hekaheka na shughuli za kichungaji, yuko njiani akipita vijiji vya Samaria na Galilaya akielekea Yerusalemu. Sote twatambua anaelekea Yerusalemu kufanya nini! Bwana akiwa katika utume huo atakutana na watu 10 wenye ukoma. Watu hawa wanaonekana kuwa na mbegu ya imani na hivi wanapaaza sauti na wanamwalika Bwana awahurumie na kuwaondoa katika shida yao.

Bwana anawapokea na anawaambia nendeni mkajioneshe kwa makuhani. Bwana anataka watu hawa wakutane na uso wa Mungu katika safari hiyo ya kwenda kujionesha kwa makuhani. Wanakutana na Mungu ambaye haogopi sura zilizoharibiwa na ukoma ndio dhambi bali Mungu anayezikumbatia sura hizo na kuzisikiliza toka moyoni mwake.

Mwinjili anataka kutufundisha kuwa kupona ni tendo la safari ya kiimani, ni tendo la kukutana na uso wa Mungu, na zaidi ya hayo, ni jambo linalojengwa katika upole na linataka pia kushirikisha jumuiya ya watu, ndiyo maana ya kuwaambia waende wakajioneshe kwa makuhani.

Mpendwa msikilizaji, mara kadhaa mantiki yetu ni kuwakwepa hawa walioharibiwa na magonjwa na hivi kuwasukumiza pembezoni, basi leo Bwana anataka tukajenge mfumo wa upendo unaokumbatia watoto wa Mungu pasipo ubaguzi kwa furaha na matumaini. Bwana akisha kuwaambia waende wakajioneshe kwa makuhani wanaondoka na huko njiani wanatakasika. Ujumbe mara moja ni kwamba kukutana na Bwana ni utakaso, ni kujikabidhi kwake ili atende apendavyo na matokeo yake ni kuwa safi.

Baada ya tendo la kutakaswa Bwana anakuja na hoja nyingine akitaka kujenga moyo wa shukrani katika kuishi imani yetu, ndiyo kusema chochote tukipatacho tuseme asante kwa yule anayetupatia na zaidi Mungu mgawaji wa mapaji yote. Ni katika mantiki hiyo Mwinjili anamweka Mkoma aliyetakasika mbele yetu, akirudi kumshukuru Bwana. Na mtakasika huyu cha ajabu alikuwa Msamaria!

Wengine ambao pengine wangesadikika zaidi kuwa wa kwanza kutoa shukrani hawakuonekana! Katika hili Bwana atajenga moyo wa shukrani lakini pia atajenga mantiki ya kuwainua Wasamaria ambao walisadikika wazushi na wasio na akili, lakini sasa badala yake wanakuwa mfano bora wa imani na shukrani kwa Mungu. Mpendwa shukrani haitegemei kumbe kabila lako bali unyenyekevu wako ukijikabidhi mikononi mwa Bwana aliyekuondoa katika uvuli wa mauti kwa njia ya ubatizo.

Tukisonga mbele katika tafakari tunaona kisha tendo hilo la shukrani basi Bwana anasema inuka uende zako imani yako imekuponya. Jambo la nguvu ambalo twapaswa kulishikilia pia katika fundisho la Bwana ni lile hasa la kuguswa na sura ya Mungu na kuweza kuangaziwa ili kuweza kutoa shukrani kwake. Katika siku zetu hizi suala la shukrani sasa linaanza kuwa adimu sana.

Kumbe kumbuka shukrani na imani havitengani kabisa. Shukrani ya Msamaria inampa Bwana nguvu ya kwenda kukabiliana kifo huko Yerusalemu. Ndiyo kusema haitoshi kusema Bwana utuhurumie bali kuongeza Bwana tunakushukuru kwa zawadi ya Imani, kwa zawadi ya ndoa yetu, kwa zawadi ya upadre, kwa zawadi ya utawa na karama nyingine zote tulizozipokea toka kwa Mungu.

Nikutakie moyo wa shukrani daima ukiimba sifa za Bwana daima kwa utenzi wa shukrani. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.