2013-10-15 08:02:15

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 26 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa


Tunaendelea kama kawaida katika kipindi chetu tafakari masomo Dominika, tayari tumekwisha safiri hadi Dominika ya 26 ya mwaka C. Katika Injili ya tunayoitafakari Mwinjili Luka anatupa mfano ambao tunawakuta watu wawili ambao ni Lazaro na yule tajiri mwenye kutumia hasa mali yake, katika maisha yao hapa duniani na baada ya maisha ya duniani kila mmoja yuko katika sehemu aliyoitayarisha. Hukumu ambayo inasimuliwa pale iko wazi na inagota pasipo kupinda katika mahali pake.

Mpendwa msikilizaji tuanze kumtazama huyu tajiri. Huyu alikuwa tajiri kwa maana halisi ya utajiri, yaani utajiri unaoonekana wazi. Katika Agano la Kale aliyekuwa tajiri kwa hakika alionekana kubarikiwa na Mungu. Si tu katika Agano hilo tu bali kwa wakati fulani katika ulimwengu wa kikalvinisti utajiri ulionekana kama baraka toka kwa Mungu.

Pamoja na hayo mawazo yaliyokuwepo Bwana wetu Yesu Kristo anakuja na hukumu na fundisho tofauti juu ya utajiri na mali kwa ujumla. Ukitazama vema huo mfano utaona kuwa huyu tajiri jambo la msingi kwake ilikuwa ni anasa, kumbe, ni kinyume na baraka toka kwa Mungu, ni kinyume na maadili na mwenendo mzima wa jamii. Inaonekana pia tajiri huyu hana hata jina wala familia ndiyo kusema hata utu ni walakini! Ni kwa namna hiyo ile hali ya kuwa katika moto ilikwishaanza hapahapa duniani! Ni hali ambayo alilipandikiza mwenyewe katika maisha yake hapa duniani.

Mpendwa mwana wa Mungu, mara moja tunaweza kujiuliza nani anaingia motoni? Kwa hakika kulingana na mfano huu ni yule ambaye amejifungia katika ulimwengu wake wa mali na anasa, mchoyo ambaye kwa hakika kumsaidia mtu kama Lazaro ni kero kubwa. Ni yule ambaye anao woga siku zote wa kupoteza mali yake na hivi hujikomaza katika uchoyo na kutafuta namna ya kulinda mali yake.

Ni yule ambaye upendo kwa wengine unaosimikwa katika moto wa mapendo ya Mungu kwa mwanadamu ni sumu au umejengeka katika mfumo wa mahesabu kama wale ndugu wa wili Kuhani na Mlawi waliompita mteswa na baadaye mteswa huyo akaja kusaidiwa na Msamaria mwema. Basi mpendwa mwana wa Mungu angalieni vema namna ambayo ni njema katika kuendesha utajiri ulionao, yaani akili, mali muda, familia nk ili ukufae kwa maisha ya uzima wa milele.

Mpendwa msikilizaji yafaa sasa tumtazame huyu Lazaro maskini wa Mungu. Kwa hali yake kimwili katika mazingira yale isingetarajiwa Bwana kumtazama. Kuna mawazo tangu wakati ule na hata hivi leo kwamba pengine hali ya umaskini inasababishwa na maskini wenyewe! Inawezekana, lakini tuangalie mfumo jamii! Pamoja na mawazo hayo Bwana analofundisho tofauti, kwake yeye maskini ni watoto wa Mungu, na amekuja kwa ajili yao, kumbuka nimepakwa mafuta ili niwahubirie maskini habari njema, Lk 4:18.

Basi mpendwa, Lazaro anatofautiana na tajiri kwanza ana jina tofauti na tajiri ambaye hana jina. Jina lake lamaanisha “Mungu ni Msaada, Mungu nisaidie”. Jambo jingine la kutazama ni kwamba Lazaro yuko kifuani mwa Ibrahimu akifurahia utukufu wa Mungu. Maana yake nini kuwa kifuani? Ni kuwa katika kitovu na kisima cha mapendo. Katika msingi huohuo wa kumweka Lazaro katika mtima wa mapendo, Bwana huwajali wale wote wanaoteseka katika ulimwengu wa leo.

Mpendwa mwana wa Mungu nini maana ya fundisho hili? Bwana ataka kuwakemea tu matajiri au ataka nini! Bwana hayuko katika mlengo wa ugomvi na matajiri bali anaonesha kuwa hali ya namna hii katika jamii ya watu haifai kuendelea yafaa kuiacha na kuishi maisha ya kugawana sawa kile ambacho Mungu amtujalia sisi sote. Anataka kuonesha kuwa hali ya kujijenga katika uchoyo yaleta hatari ya kukosa zawadi za Kimungu.

Bwana anakuja na dunia mbili zilizotengana kwa mtalo mkubwa na yanajitokeza mawazo ya kutuma mmoja toka ulimwengu wa Lazaro ili akawape habari walioko duniani wakatubu! Jibu kuhusu mawazo hayo ni kwamba wanao Musa na manabii, wanayo sheria wakafuate hayo na watafika katika furaha kamilifu.

Mpendwa, hawa ambao wanao manabii na sheria ni akina nani? Ndio sisi katika ulimwengu wa leo. Tunaalikwa na tunapaswa kushika vema mausia ya Bwana. Tunaalikwa kugawana sawa mapato yetu, kuishi maisha ambayo yatupa jina tofauti na tajiri ambaye hana asilia, hana jina, hana familia! Tuwatazame wale ambao wanatamani kushibishwa kwa makombo na mabaki, ambao wanaishi katika mitaa ambayo haiendani na hadhi ya mwanadamu aliye kiumbe cha Mungu.

Ninakutakia furaha na amani itokayo katika maisha ya ushirika mtakatifu katika kujenga familia ya Mungu. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.