2013-10-15 07:57:54

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 25 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa


Ni mara nyingine tena tunakutana katika meza ya Neno la Mungu ambayo ni hai daima na hutulisha na kutushibisha. Ni Dominika ya 25 ya mwaka C. Neno latufunda kuwa wenye hekima katika kutafuta ufalme wa Mungu.

Injili tunayoitafakari ni Injili inayotupa ugumu kwa namna moja au nyingine. Bwana anamsifu huyu mtu ambaye alikabidhiwa mali ili aweze kuisimamia na badala yake anashindwa akijiimarisha katika ubadhirifu wa mali hiyo ya tajiri wake.

Sasa tunajiuliza Bwana aweza kusifu udhalimu? Hapa, Bwana anataka kujenga hoja ya kuwa mwenye Hekima katika kuongoza maisha yako. Anasifu uerevu wa ndugu huyu katika kutatua shida itakayopmpata baada yakuondolewa katika mamlaka yake. Ndiyo kusema mfuasi wa Bwana lazima awe mwerevu katika kuongoza maisha ya kikristu.

Bwana anasema hilo akitaka kusema kuna baadhi ya wana wa nuru yaani ambao tayari wanafahamu nini maana ya nuru lakini hawana uwezo kama huyu mfanyakazi dhalimu, ndiyo maana an asema wana wa ulimwengu huu huwa na busara hata kuliko wana wa nuru. Kuwa na uerevu maana yake daima kupambanua nyakati na mahitaji kulingana na mpango wa Mungu.

Mpendwa msikilizaji katika mfano uliotolewa na Bwana yule mfanyakazi dhalimu ni mwerevu kwa maana ya kutunza nafasi yake katika jamii hapo baadaye, yaani anatazama faida yake wakati huo akibomoa nafasi ya tajiri mwajiri wake. Huyu ndugu tunaweza kusema anao uwezo mkubwa kiakili na hasa katika ngazi ya utendaji (matendo). Anapungukiwa jambo moja tu nalo ni lile la kutuzama maisha ya mbeleni wakati kutakuwepo na hukumu kwa wote.

Wakati huo atawajibika kujibu hasara yote aliyoisababisha katika uongozi wake. Jambo jingine linalofuata ni lile linalotokana na mazoea, yakwamba amekwishazoea kutengeneza mbinu za wizi basi mazoea haya hayaruhusu mtu kumtumikia Mungu kiurahisi! Mazoea ya utajiri na mali ni gereza mojawapo kati ya magereza mbalimbali, huondoa uhuru kamili katika kuhangaikia uzima wa milele.

Bwana anatutaka sasa tuelewe anapoenda hatua ya pili kwamba mali tuliyonayo kama hatutaifanya miungu basi itaweza kusaidia maendeleo ya mwanadamu. Chamsingi mali hii isiwe ndo mwisho wa upeo wa macho na mioyo yetu.

Wakati tukiwa huru toka utumwa huu wa mali basi tunakuwa tumepata nafasi ya kutangaza habari njema kwa wepesi na ushujaa zaidi. Mali iliyokusanywa pasipo haki hujenga kuta za utengano na mali ambayo hugawanywa kati ya watu kwa upendo hujenga mshikamano katika maisha ya watu. Mshikamano huu hufikisha familia nzima katika uzima wa milele.

Mpendwa msikilizaji kuweni imara katika kutambua hekima ya Kimungu katika kuongoza mali ulizonazo ili kusudi ziwe kwa mafaa ya wokovu. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.