Siku ya Baba wa Taifa na changamoto kwa watanzania!
Serikali ya Tanzania itajenga kituo cha kuwaenzi waasisi wa taifa katika eneo la Kiromo
Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani ambapo tayari upembuzi yakinifu umefanyika. Kauli
hiyo ilitolewa Mjini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi
wa Umma, Celina Kombani katika mkutano wa hadhara wa kuadhimisha miaka 14 ya kumbukumbu
ya kifo cha Baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yaliyofanyika katika
viwanja vya Nyerere Square.
Waziri Kombani alisema licha ya kupata eneo hilo
tayari upembuzi yakinifu umefanyika na athari za kimazingira ambapo pamoja na mambo
mengine kituo hicho kitafanya kazi ya kuzifanya, kuhifadhi kumbukumbu, mali na vitu
vyenye umuhimu wa kihistoria vya waasisi hao. Alisema kituo hicho pia kitaratibu shughuli
zote zinazohusu waasisi ikiwemo kuhamasisha umma kuhusu utafiti, kuandaa machapisho
mbalimbali yanayoelezrea michango na kazi mbalimbali walizowahi kufanya waasisi hao.
Waziri
Kombani alisema umedhihirisha mataifa mengi duniani yana utaratibu wa kisheria
na kisera wa kuebnzi na kuhifadhi kumbukumbu za viongozi wao mashuhuri. Alisema
katika kufanikisha hilo serikali imeazimia kuweka utaratibu wa sheria wa namna ya
kuendesha kusimamia na kuratibu shughuli za kuwaenzi viongozi wakuu waasisi wa
taifa kwa kuhifadhi vielelezo vya kumbukumbu zao kwa manufaa ya taifa na vizazi
vijavyo.
“Heshima, utu, amani na utulivu, demokrasia na maendeleo ya Mtanzania ni
urithi na utajiri wa taifa letu ambao umetokana na juhudi na mchango mkubwa wa
kujitoa mhanga kwa viongozi wetu hawa hivyo hakuna budi kuyalinda kwa kuwaenzi”
alisema
Alisema mwaka 2004 sheria ya kuwaenzi waasisi wa taifa namba 18 ya mwaka
2004 ilipitishwa na bunge kwa lengo la kuweka utaratibu wa kuendesha, kusimamia
na kuratibu shughului za kuwaenzi waasisi wa taifa Mwalimu Nyerere na hayati Abeid
Aman Karume na kuhifadhi vitu na kumbukumbu zao kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.
Aidha alisema serikali imefanikiwa kuzitambua taasisi , asasi zinazomiliki kumbukumbu,
mali na vitu vyenye umuhimu wa kihistoria kitaifa ili kuhakikisha zinatunzwa vizuri
kwa maslahi ya taifa.
Alibainisha kuwa serikali imeunda bodi ya udhamini wa
mfuko wa kuwaenzi waasisi wa taifa ambayo itakuwa na jukumu la kutafuta, kukusanya
na kusimamia fedha za mfuko huo.
Kwa upande wake, Balozi mstaafu Job Lusinde
alisema Mwalimu Nyerere alikuwa mwanasiasa mwenye kipaji cha pekee alimini kuwa
siasa kwake ni kuwatumikia watu waliokuamini na kukupa dhamana ya kuwaongoza. Alisema
kutokana na msingi huo mwalimu alikuwa ni mwanasiasa mwenye maono ya mbali hasa
ukizingatia kuwa matukio ya watu aliokuwa akiwaongoza yalimuumiza na aliguswa nayo
kutoka moyoni akiamini, kuhubiri na kuenenda katika umoja.