Kardinali Luis Antonio Tagle, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila nchini Ufilippini
anasema, Jimbo lake kwa sasa linajiandaa kwa ajili ya kuadhimisha Kongamano la Kijimbo
kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu
Mstaafu Benedikto wa kumi na sita, kama sehemu ya kumbu kumbu ya Jubilee ya Miaka
50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Kumbu kumbu ya Miaka 10 tangu Mwenyeheri
Yohane Paulo wa Pili aliposchapisha kwa mara ya kwanza Katekesimu Mpya ya Kanisa Katoliki.
Huu ni muhtasari wa Imani, Sakramenti za Kanisa, Amri za Mungu na Maisha ya Sala.
Kardinali
Tagle ni mmoja wa Makardinali wenye umri mdogo sana, ikilinganishwa na Makardinali
wengine anasema kwamba, inasikitisha kuona kuwa, nchini Ufilippini ambako imani ya
Kikristo ilikuwa imeota mizizi katika sakafu ya maisha ya waamini lakini leo hii,
wamekengeuka na wanaanza kushikwa na ubaridi wa maisha ya kiroho.
Hii ndiyo
hali ambayo inajitokeza kwa kasi kubwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo
ya sayansi na teknolojia, kiasi kwamba, Mwenyezi Mungu hana tena nafasi katika maisha
na vipaumbele vya watu. Hali hii imeenea sana kwa nchi za Ulaya na Amerika, lakini
pole pole ubaridi wa maisha ya imani na maadili unaanza kupenya sehemu mbali mbali
za dunia.
Idadi ya Wakristo nchini Ufilippini ilikuwa ni kubwa katika kipindi
cha miaka michache iliyopita, lakini kwa sasa hali inazidi kudidimia mwaka hadi mwaka,
kwani idadi ya Wakatekumeni wanaobatizwa na Wakristo wanaofunga ndoa Kanisani inazidi
kuongezeka kwa kasi ya kushangaza. Kwa miaka kadhaa sasa kuna baadhi ya wakristo hawauoni
tena mlango wa Kanisa hasa katika Ibada za Jumapili na Siku kuu zilizo amriwa.
Baadhi
yao wameamua kujiunga na Madhehebu mengine ya Kikristo wakitumainia kupata muujiza
wao! Hizi ndizo changamoto ambazo Kanisa Katoliki nchini Ufilippini inakumbana nazo
na sasa limeamua kuanza kuchemsha dawa inayofumbatwa katika mchakato wa Uinjilishaji
mpya. Dunia inaendelea kubadilika kwa kasi, lakini Neno la Mungu linabaki pale pale,
ni jukumu la Kanisa kuendelea kuinjilisha ili hatimaye, Neno la Mungu liweze kuota
mizizi katika maisha na vipaumbele vya waamini kwa kutoa majibu muafaka kwa changamoto
mamboleo.
Kardinali Tagle anasema, kuanzia tarehe 16 hadi tarehe 18 Oktoba,
Jimbo kuu la Manila litaadhimisha Mwaka wa Imani, kama sehemu ya mchakato unaopania
kuwahamasisha waamini kuonja tena ndani mwao ile furaha ya imani, ambayo wanapaswa
kuikiri, kuiadhimisha, kuimwilisha katika maisha adili na kuisali. Kongamano hili
linatarajiwa kupata wawakilishi kutoka katika nchi kadhaa za Asia.
Huu ndio
utakaokuwa mchango wa Kanisa Katoliki nchini Ufilippini katika Maadhimisho ya Mwaka
wa Imani, utakaohitimishwa katika Maadhimisho ya Sherehe ya Kristo Mfalme.