2013-10-15 10:10:17

Kuna matajiri wakubwa Afrika, lakini watu wengi bado wanalia na janga la umaskini!


Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, pengo kati ya matajiri na maskini Barani Afrika limeongezeka kwa kiasi kikubwa. Hali ya maisha imeendelea kushuka kutokana na watu wengi kutumbukia au kutumbukizwa katika lindi la umaskini wa hali na kipato kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha. Hata katika hali kama hii, kikundi cha watu wachache Barani Afrika kimeendelea kucharuka kwa kuwa na uwezo mkubwa kiuchumi, kati yao kuna hata wanawake, jambo ambalo limewaacha wengi kushika tama kwa mshangao mkubwa!

Uchunguzi uliofanywa na Jarida moja linalochapishwa nchini Nigeria linaonesha kwamba, kikundi hiki cha watu wachache Barani Afrika, kinamiliki walau kiasi cha dolla za kimarekani zipatazo billioni 143, 88. Hii ndiyo sura mpya ya Bara la Afrika ambalo linaendelea kucharuka katika maendeleo ya vitu, lakini hali ya Waafrika wengi bado ni “janga la kitaifa”. Maendeleo ya vitu yamewaacha wananchi wengi katika hali ya umaskini, jambo linalotishia amani na utulivu katika nchi nyingi Barani Afrika. Kuna baadhi ya watu ndani ya Jamii wanatumia umaskini wa watu kwa ajili ya mafao yao binafsi.

Takwimu zilizotolewa na Benki ya dunia kuhusu hali ya umaskini duniani, zinaonesha kwamba, katika kipindi cha miaka thelathini iliyopita, uchumi wa Bara la Afrika umeendelea kukua, lakini idadi ya wananchi Barani Afrika wanaoishi katika hali ya umaskini wa hali na kipato imeongezeka maradufu kutoka watu millioni 205 hadi kufikia watu millioni 414.

Takwimu zinaonesha kwamba, matajiri wengi wa Bara la Afrika ni wale ambao kwa kiasi kikubwa utajiri wao umetokana na nafasi zao katika masuala ya kisiasa. Bwana Aliko Dangote ni kati ya matajiri wakubwa Barani Afrika. Anamiliki viwanda vya kutengeneza sementi, viwanda vya sukari na chumvi na kwamba, utajiri wake ni sawa na dolla za kimarekani billioni 20.2.

Nigeria ni kati ya nchi za Kiafrika inayoongoza kwa kuwa ni idadi kubwa ya matajiri Barani Afrika. Kati ya matajiri wakubwa 55 Barani Afrika, 20 ni wale wanaotoka nchini Nigeria. Afrika ya Kusini ina matajiri wakubwa 9 na Misri inao matajiri 8.

Mama Ngina Jomo Kenyatta, Mjane wa Rais Jomo Kenyatta wa Kenya na Mama yake mzazi wa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ni kati ya matajiri wanawake kutoka Barani Afrika. Anafuatiwa na Isabel Dos Santos, Binti mkubwa wa Rais Dos Santos wa Angola na mwanamke wa tatu ni Folorunsho Alakjia ambaye utajiri wake ni sawa na dolla za Kimarekani billioni 7.3 unaotokana na uwekezaji katika sekta ya nishati na katika sekta ya mitindo ya mavazi.

Hii ndiyo picha ya kucharuka kwa uchumi Barani Afrika, kunakoendelea kuwatumbukiza wengi katika “majanga ya umaskini wa hali na kipato”. Waswahili wanasema, inawezekana kujikwamua kutokana na umaskini kwa kuwekeza zaidi na zaidi katika sekta ya elimu, ili hata watoto wa wakulima waweze kujikwamua. Inawekana ikiwa kila mtu atatekeleza wajibu na dhamana yake katika Jamii.








All the contents on this site are copyrighted ©.