Papa Francisko afafanua kwa nini Kanisa ni Katoliki la ulimwengu
Katika katekesi yake ya kila Jumatano, kwa wiki hii Papa Francisko amezungumzia juu
ya Kanisa na hasa akieleza maana ya Kanisa kuitwa Katoliki, kama tunavyokiri katika
sala ya Nasadiki, Nasadiki katika kanisa moja takatifu Katoliki la ulimwengu.
Papa
amesema neno Katoliki, awali ya yote linatokana na neno la Kigriki
' kath'olòn ' maana yake ni kulingana wote kwa ujumla.
Papa
aliendelea na mafundisho yake, lakini kwanza alihoji, ina maana gani kusema kanisa
katika ujumla wake(katoliki)’ au pia kwetu sisi ina maana gani kusema Kanisa ni
la ulimwengu?
Papa Francisko alitoa ufafanuzi kwa kuelezea misingi mitatu
ya kanisa kuwa la ulimwengu akisema, awali ya yote –tunasema Kanisa Katoliki ni kwa
sababu ni mahali au jengo lililo mahali popote kwa ajili ya kutangaza imani kwa
Yesu Kristu, aliye mletea wokovu binadamu, imani inayo tangazwa kwa watu wote bila
ubaguzi. Kanisa ni mahali watu wote wanaalikwa kukutana na huruma ya Mungu, ambayo
humbadili mtu, kwa kuwa ndani mwake yumo Kristu , zawadi ya kweli katika kuikiri imani
, na ni utimilifu wa maisha ya kisakramenti na ukweli wa fumbo la mwili uliotolewa
kwetu. Katika Kanisa , kila mmoja wetu ni muhimu kwa ajili ya imani, katika kuyaishi
maisha ya Kikristu , katika kuwa watakatifu , na katika kutembea kila mahali na
katika kila wakati.
Papa alieleza “Kanisa ni sawa na maisha ya familia, ambamo
kila mmoja wetu huutolea uwepo wake kwa ajili wanafamilia, na ni mahali panapo ruhusu
binadamu kukua, kukomaa na kuishi. Hakuna anayeweza kukua akiwa peke yake, au kutembea
katika safari ya maisha akiwa peke au kujitenga mbali na wengine, bali sote hukua
katika mjumuiko wa watu. Na ndivyo ilivyo kwa Kanisa. Katika Kanisa kwa pamoja tunasikiliza
Neno la Mungu , tukiwa na uhakika kwamba ni ujumbe toka kwa Bwana alotupatia, ndani
ya Kanisa tunaweza kukutana na Bwana katika Sakramenti alizotupatia kama madirisha
yaliyo wazi kwa ajili ya kuupitisha mwanga wa Mungu, na miito, na pia ambamo tunaweza
kuchota maisha ya Kimungu”.
“Katika Kanisa tunajifunza kuishi katika ushirika
na kwamba upendo hutoka kwa Mungu. Mmoja wenu leo hii anaweza kuuliza kwa jinsi gani
mimi ninaweza kuishi ndani ya kanisa? Je ni tu katika kushiriki maisha ya jamii au
kwenda kanisani au kujifungia mwenyewe na matatizo yangu, au kujitenga mwenyewe na
wengine? La sivyo , katika maana hii ya kwanza kwa nini Kanisa ni Katoliki,ni kwa
sababu Kanisa Katoliki ni nyumbani kwa kila mtu, sisi sote ni wana wa Kanisa na
wote ni wakazi wa nyumba hiyo Kanisa “.
Papa aliendelea kutaja maana ya pili
ya Kanisa kuwa Katoliki akisema ni kikatoliki kwa sababu ni zima linalo endelea
kuwepo duniani kote kwa ajili ya kutangaza injili kwa kila mwanamme na kila mwanamke
. Kanisa sio kundi la wasomi , wala si kwa ajili ya watu wachache. Kanisa halina
mpaka, ujumbe wake hupekwa kwa watu wote, jamii nzima ya wanadamu. Kila mtu anaweza
kusema: Parokia yangu ni Katoliki , kwa kuwa hiyo ni sehemu ya Kanisa zima la ulimwengu
, ambamo mna ukamilifu wa zawadi ya Kristo, imani, sakramenti na huduma katika ushirika
na Askofu, na Papa, ni wazi kwa wote bila ubaguzi .
Mwisho, Kanisani Katoliki
kwa sababu ni Nyumba ya Mapatano, ambamo na katika hali ya tamaduni na lugha huchanganyika
pamoja na kuwa kitu kimoja chenye utajiri wa kipekee. Papa alieleza na kutoa mfano
wa kinanda, ambamo vifungo vyake vinaposhikwashikwa kwa namna moja ya makubaliano
na maelewano, hutoa muziki muzuri wa kuvutia kucheza pamoja.
Papa alieleza
na kumtaka kila mmoja , kumwomba Bwana atufanye sisi sote kuwa wakatoliki, kama familia
inavyokua pamoja katika imani na upendo, pia kuwavutia wengine katika umoja wa kanisa,
na kupokea zawadi na sadaka ya kila mmoja, kwa ajili ya kumtukuza Mungu kwa pamoja
kwa wema wake , neema zake na wokovu wake wa upendo.
Baada ya Katekesi, Papa
alitoa salaam zake kwa makundi ya watu waliofika kumsikiliza.