2013-10-09 15:18:20

Miaka kumi tangu kutangazwa Mtakatifu Daniel Comboni


Wakati Mama Kanisa anapoadhimisha miaka kumi tangu kutangazwa mtakatifu Daniel Comboni, shirika la Wamissionari wa Comboni wa Moyo wa Yesu wanasema wanayo sababu ya kuyasheherekea maisha ya Mtakatifu huyu ambaye aliweka jiwe la msingi la maisha yao ya kimissionari.

Kwenye makala yaliyoandikwa na Mkuu wa shirika hilo, Padre Enrique Sanchez Gonzalves, na kuchapishwa na gazeti la Kila siku la Osservatore Romani la Roma, shirika hilo linasema ni wakati muafaka wa kuadhimisha kwa furaha utakatifu wa mtu aliyeyatoa maisha yake bila ya kujibakiza kwa ajili utume wa kimissionari. Daniel Comboni aliufungua moyo wake na kumwachia Mungu kuuongoza alipopenda yeye Mungu, na hivyo kuweza kutwaliwa kwenye nchi geni ambapo aliishi na kutoa huduma ya kitume hadi mwisho wamaisha yake.

Anasema Padre Enrique kwamba Comboni aliupokea mpango wa Mungu na kuwa mwaminifu, katika kuufuata na kuisoma hadithi ya mwanadamu akitumia macho ya Mungu. Uaminifu huo ndio ulioelekea kuchipuka kwa familia ya Wakomboni ambao hata leo wanaendelea kujitolea kidete kwa ajili ya wokovu wao na wa ndugu zao sehemu mbalimbali duniani.

Kwa ajili ya majitoleo ya Comboni, anasema Padre Generali wa shirika la WaComboniani, Wanachama wake wamefahamu kwamba utakatifu unawezekana ikiwa kuna mshikamano wa nia, na kujibiidisha kwa pamoja kwa ajili ya wana wapenzi wa Mungu wanaokumbwa na changamoto mbalimbali na wenye kusukumizwa pembezoni mwa jamii.

Anasema pia kwamba utakatifu unawezekana pale penye unyenyekevu na unyofu katika kuendeleza mshikamano na dunia yenye kuyajali maslahi na haki za wanyonge, na hata kwa kukubali kuhudumu kwenye maeneo ambayo wengi wasingependa kufanya kazi.

Ni wakati pia wa kuukumbatia msalaba huku wakitambua kwamba mbegu za utakatifu pia hukua chini ya msalaba, na kwamba maisha ya mmissionari sio ya kutafuta faida yake mwenyewe au starehe, hadhi, ustawi na raha maishani, vitu ambavyo vinazidi kupewa kipaumbele licha ya mateso mengi yanayowakumba wengi wanaosahaulika na jamii. Ila maisha ya umissionari humhitaji mhusika kutopenda kupewa heshima au kutafuta maslahi yake mwenyewe, na badala yake, kama alivyofanya Mtakatifu Comboni, kuwa tayari kutumiwa na Mungu kwenye mpango wake wa kuwaongoa watu wake.

Kuukumbatia utakatifu wa Comboni kunamaanisha kukubali kutemebea kwenye njia ya msalaba kujitoa sadaka, kusali, na kufuata mantiki ya Mungu na sio ile ya binadamu. Ni kupokea kwa unyenyekevu neema na huduma ya utakatifuzaji na kumwachia Kristokuyatawala maisha, anasema Padre Enrique.

Padre huyu pia amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwachangamotisha maaskofu, Mapadre na wote wenye kuhudumu ndani ya Kanisa kuwa wachungaji wema wenye kuitambua harufu ya kondoo wao, ambayo pia ndiyo harufu ya utakatifu wao.











All the contents on this site are copyrighted ©.