Mafundisho ya Papa, kufanya upya Mji wa Assisi, Asema Meya Claudio Ricci
Kwenye ziara yake ya kichungaji mjini Assisi siku ya Ijumaa, Baba Mtakatifu Francisko
alikaribishwa na maneno ya Meya wa Assisi, Bw. Claudio Ricci ambaye alisema kwamba
maeneo aliyoishi Mtakatifu Francisko ni urithi kwa ajili ya majadiliano ya kibinadamu,
na kwamba sasa mawe yaliyo hai yataanza kuishi maisha mapya kutokana na mwanga mpya
unaomulikwa na ziara ya Papa Francisko mjini humo. Meya Claudio Ricci amemshukuru
Papa Francisko kwa kukitembelea kwanza kituo cha wallemavu cha Serafiko, huku akisema
kwamba ni ishara kwamba Papa ameukumbatia moyo wa Kifrancisko, wa kuwajali na kuwaonyesha
mapendo yaliyojaa huruma, watu walio wanyonge zaidi kwenye jamii; ishara pia ya Kanisa
lililojaa mapendo na huruma, na moyo wa kushirikishana mapendo hayo. Amesema Meya
huyo kwamba siku ya ziara ya Papa Francisko mjini humo itabaki kama kumbukumbu hai
kwani inawawezesha watu wengi kuelewa maana ya kujitoa bila ya kujibakisha kwa ajili
ya hadi na heshima ya binadamu wengine. Amemshukuru Papa pia kwa mafundisho yake
ambayo yanaendelea kuwachangamotisha na kuwapa matumaini mapya yaliyojengwa juu ya
unyenyekevu watu wengi kote duniani, huku akisema kwamba mji wa Assisi hautabaki ule
wa zamani, kwani baada ya kuondoka mjini humo zawadi ya mafundisho yake Papa yataendelea
kuupyaisha mji huo, upya ambao utakuwa kiini cha mazungumzo mapya ya jumuia ya kibinadamu.
Ni ziara ya kwanza ya kichungaji mjini Assisi inayofanywa na Papa ambaye amelichagua
jina la Mtakatifu huyo wa Assisi na kuikumbatia roho ya mtakatifu huyo aliyeishi kwenye
Karne ya 12 na13.