2013-10-04 14:28:12

Buea Mwenyeji wa kilele cha Maadhimisho ya Mwaka wa Imani - Cameroon


Jimbo la Bueu limeteuliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Cameroon, kuwa mwenyeji wa Maadhimisho ya Kitaifa ya kufunga mwaka wa imani. Shamra shamra za maadhimisho haya zimeanza Alhamis Octoba 3, 2013, na inategemewa zaidi ya mahujaji elfu sita kutoka pande mbalimbali za Cameroon wakiongozwa na Maaskofu wao 33 watashiriki katika kilele cha maadhmisho haya.

Kwa ajili hiyo, Tume ya Maandalizi ya sherehe hizi, imetenga mahali maalum katika Kanisa Kuu la Katoliki la Small Soppo, kwa shamrashamra hizi. Inakumbukwa tarehe 21 Septemba 2013, Askofu wa Bueu alikutana na wanahabari na umma kwa ujumla kueleza nini maana ya sherehe hizi za Kanisa. Na alisema, Imani ni zawadi kutoka kwa Mungu , na kupitia Imani, waumini huungana na Mungu.

Na kwamba , Yesu Kristu aliitoa zawadi hii kwa binadamu bure ya kuwa pamoja na Mungu. Lakini pale imani inapokosa , binadamu huvunja uhusiano wake na Mungu. Na ndiyo maana kanisa linatoa wito kwa watu wote kuishi na imani kwa Kristu, ili wawe katika umoja kamili na Mungu. Basi Mwaka wa Imani, Askofu Bushu aliendelea kusema, ulilenga kuamsha upya imani kwa Kristu, hasa ambao waliokuwa wamejiweka mbali na Mungu kutokana na mabadiliko ya kidunia. Mambo mengi sasa yanafanyika na kututenga na Mungu. Tunamezwa na mambo ya kidunia lakini sasa tumesema basi yatosha .

Hivyo sherehe hizi za kuufunga Mwaka wa Imani, zinafungua kipindi kipya cha imani thabiti kwa Kristu, hasa katika kupambana na changamoto zote zinazotaka kumtenganisha na Mungu , alisisitiza Askofu wa Buea.

Shughuli za Kilele cha kuufunga mwaka wa Imani , zinaongozwa na Mjumbe wa Kitume wa Papa nchini Cameroon, Askofu Mkuu Piero Pioppo. Kati ya matukio yatakayofanyika ni pamoja na uwepo wa warsha , semina na makongamano yanayolenga kuwa na hoja za kuimarisha imani ya Kikristu. Na kai ya wageni waalikwa ni pamoja na Mratibu wa kanisa la Presbyterian Cameroon, naKatibu Mkuu wa Kanisa la Baptist Cameroon.








All the contents on this site are copyrighted ©.