Kanisa Katoliki Burkinafaso, halitatuma wajumbe katika Seneti
Ouagadougou (Agenzia Fides) – Kanisa Katoliki nchini Burkina Faso limesema halitatuma
wajumbe kuliwakilisha kwenye bunge Senate la nchi hiyo. Kwa tamko hilo, Baraza la
Maaskofu Katoliki la Burkina Faso limekatalia mbali pendekezo la sheria ya nchi hiyo
iliyopitishwa mwezi Mei ambayo inawania kuyapa nafasi kadaa makundi ya kidini kutuma
wajumbe kwenye bunge la nchi hiyo. Wabunge hao wangechaguliwa na viongozi wa kidini
ili kuweza kuwasilisha maslahi ya dini zao.
Hata hivyo, Baraza la Maaskofu
Katoliki nchini humo linasema kwamba Kanisa Katoliki litaendelea kusimama na ukweli
wa mafundisho yake, kamwe haliwezi kwenda kinyume na msimamo wake kwa kuwatuma wawakilishi
kwenye uongozi wa kisiasa, na kwamba maaskofu hao wataendelea kutekeleza wajibu wao
wa kutoa mwelekeo na msimamo wa Kanisa hata kuhusiano na mambo ya uongozi, bila kujihusisha
kisiasa kwa kuwapeleka wawakilishi maalum.
Lengo la Kanisa ni kuendeleza mshikamano
na amani kwenye jamii ya wananchi wote na hata kama kuna lazima, kusimama na upinzani
ikiwa utakuwa unasimamia haki na mafao ya wananchi wote.
Mwezi Julai Maaskofu wa
nchi hiyo walipinga vikali kuanzishwa kwa Bunge la Senate nchini humo, wakihofia kwamba
jambo hili huenda likaathiri amani nchini Burkina faso.