2013-09-21 08:03:33

Jinsi ilivyo vyema na kupendeza, ndugu kuishi pamoja kwa amani..


Maana ya Uchungaji ni kulipokea kundi la Mungu kwa ukarimu mkuu, kutembea nalo na kubaki pamoja nao.

Kwa maneno hayo Baba Mtakatifu Francisko amewachangamotisha Maaskofu wapya kutoka Amekani Kusini na bara Asia aliokutana nao mjini Vatikan siku ya Alhamisi. Hii ilikuwa ni siku ya mwisho ya mkutano wa Maaskofu wapya 26 kutoka mabara hayo mawili. Mada ya Mkutano huo ilikuwa: Jinsi ilivyo vyema na kupendeza, ndugu kuishi pamoja kwa amani. ยป (Zab 132,1).

Akiongea na wachungaji wenzake, Baba Mtakatifu amesema kwamba maana ya uchungaji ama kupokea kundi kwa ukarimu ni kuhakikisha kwamba mioyo ya wachungaji inakuwa na utayari wa kuwapokea watu wote wanaokutana nao katika safari ya utume wao. Amewahimiza kuhakikisha kwamba watu wote wanapata mapokezi na ukarimu kwenye maparokia na kanisa kwa ujumla kama vile Mungu mwenyewe alivyo mkarimu wa kuwapokea na kuwakaribisha watu wake.

Kutembea na kundi, asema Baba Mtakatifu, ni wito wa kwanza wa Askofu. Askofu anapaswa kuwa ndani ya kundi, na pamoja na kundi lake. Hii inamaanisha kuwa Askofu ni lazima ashiriki kwenye furaha, matumaini, shida na mateso ya ndugu zake, kama baba aliye na uwezo wa kuwasikiliza, kuwaelewa, kuwasaidia na kuwaonyesha njia watoto wake na kutembea nao kwa mapendo.

Baba Mtakatifu pia amewachangamotisha maaskofu hao kushirikiana kwa karibu kabisa na mapadri wa majimbo yao ili kuweza kuifanikisha kazi ya kuieneza injili ya Bwana. Ni katika mshikamano huo ambapo Askofu anaweza kuwafahamu na kuwasaidia mapadri wake katika kazi yao ya kitume, kama afanyavyo mchungaji mwema. Yote haya wayafanye kwa moyo wa unyenyekevu na uaminifu mkuu, anasema Papa.

Mwisho kabisa Baba Mtakatifu anawachangamotisha Maaskofu hao wapya kubaki pamoja na kundi, kwenye majimbo yao, huku wakijiepusha na safari zisizo na lazima na vivutio vya ulimwengu wa utandawazi.

Kubaki na kundi ni kuwa daima na nafasi kwa ajili ya watu wa Mungu. Papa amewaomba maaskofu hao wapya kuhakikisha wanabaki kwenye majimbo yao bila ya kupenda kukosekana humo kwa muda mrefu bila sababu za maana. Amewaomba kutopenda kusafirisafiri bila sababu za msingi hata kama usafiri wa siku hizi umerahisishwa.








All the contents on this site are copyrighted ©.