2013-09-19 10:38:06

Askofu Shao asema, hali ya Padre Anselmo bado ni mbaya.


Askofu Augustine Shao, wa Jimbo Katoliki Zanzibar, Jumanne (18 Septemba 2013), aliieleza hali ya Padre Anselmo Mwanagamba kuwa bado ni mbaya, kutokana na tindikali aliyomwangiwa, kupenya hadi chini ya ngozi. Na hivyo wanatazama uwezekano wa kumpeleka katika hospitali zenye utalaam zaidi, ikiwezekana nje kama India, ambako kuna uzoefu wa kutosha kwa matatizo kama hayo.Hayo alieleza Jumanne katika mahojiano na shirika la habari la Fides na kunukuliwa na CISA.

Padre Anselmo Mwanga'mba, Padre wa Kanisa Katoliki Zanzibar, kwa wakati huu amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kitaifa ya Muhimbili, ambako alihamishiwa tokea Hospitali ya Mnazi mmoja Zanzibar alikolazwa baada ya kumwagiwa tindikali na watu wasiojulikana. Padre Anselmo alishambuliwa wakati akitoka katika kituo cha Internet Ijumaa iliyopita.

Padre Anselmo ni mhanga wa mashambulio mfululizo ya kutumia tindikali, yalitokea katika kisiwa cha Zanzibar katika miezi ya karibuni. Waathirika wengine ni pamoja na mabinti wawili raia wa Uingereza, waliofika Zanzibara kama walimu wa kujitolea, na pia Fadhil Suleiman , Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar.

Askofu Shao anasema , Suala la mashambulizi haya ni tata, kwani tangu mwaka jana, wameshuhudia matukio makubwa ya maonevu na dhuluma kwa Kanisa Katoliki na Wakristu kwa ujumla Zanzibar. Askofu Shao, ameeleza kwa kukumbuka matukio mengine ya Mapadre kushambuliwa, Padre Mkenda Ambrose alijeruhiwa vibaya wakati wa Siku Kuu ya Krismasi mwaka jana, ambaye hali yake bado si nzuri , na Februari mwaka huu Padre Evarist Mushi, aliuawa na watu wasiojulikana wakati akielekea kuadhimisha Ibada ya Misa. .

Askofu Shao, ametaja sababu kadhaa za unyanyasaji huo kwamba ni pamoja na mivutano ya kisiasa juu ya Katiba mpya na kuibuka kwa vikundi vinavyotaka Zanzibar iwe nchi huru kamili, badala ya kushikamanishwa na Tanganyika, pia kuna kutoelewana juu ya marekebisho ya orodha ya wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi 2015. Na kwa mtazamo wa athari za kiuchumi kijamii, ipo hisia kwamba wageni toka bara na mataifa mengine kama Kenya , wengi wao wakiwa Wakristu, wanapokonya nafasi za kazi kwa Wazanzibar. Na hatimaye kuna Waislam wenye msimamo mkali, ambao hupigia debe propaganda inayoenezwa kichinichini na wageni wenye kutoa mafunzo ya mahubiri , yenye kueneza chuki dhidi ya wakristo, hasa kwa vijana wa Kiislamu wa visiwani humo. Vijana hao walipelekwa mafunzo nje ya nchi na sasa wanaigiza moyo na mawazo ya chuki na fitina Zanzibar, kupitia mihadhara na vyombo vya habari mahalia..

Amesema, kwa kifupi , sababu za matendo maovu ni nyingi. Na hali ni ngumu, lakini hana uhakika kama Wakristu na hasa Wakatoliki ni walengwa au wanatumika tu kama chambo katika sababu hizo. Mbali na kushambuliwa Mapadre, pia , makanisa 4 yameharibiwa vibaya, amehitimisha Askofu Shao , na kunukuliwa na Fides siku ya Jumatano.

Kufuatia tukio la Ijumaa, watu 15 wanasadia polisi kuupata mtandao wa watu wanaofanya vitendo hivi viovu. Na kuna hisia kwamba , yao ni wanachama wa kikundi cha uhalifu cha Somalia cha al Shabab,a mbacho ni tawi la al Qaeda, kikundi cha kighaidi cha kimataifa.








All the contents on this site are copyrighted ©.