2013-09-18 14:14:35

Kanisa ni mfano wa Mama, asema baba Mtakatifu Francisko


Mama Kanisa ni mfano wa mama wa nyumbani anayehangaikia watoto na familia yake huku akijitoa bila ya kujibakiza kwa mafao yao. Kunayo mengi ambayo Mama kanisa anaweza kujifunza kwa mfano wa maisha na matendo ya akina mama. Ni mkazo uliowekwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye katekesi yake siku ya Jumatano alipokuwa akizungumza na halaiki ya waumin na mahujaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia waliomiminika kumsikiliza Papa kwenye uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatikan.

Baba mtakatifu alitaka kuonyesha yale akina mama wengi wanayoyatenda, wanayoyaishi na wanayoteseka nayo, kwa ajili ya watoto wao.

Ni mambo gani hayo ambayo huyafanya mama yeyote yule?

Mama humfunza mtoto wake kutembea, kujitunza na kujitegemeza na kufuata njia ifaayo maishani mwake na imwezeshayo kukua. Yote haya huyafanya na upendo mkuu, huku akifahamu fika lipi lililo jema kwa manufaa ya mtoto wake, mambo ambayo sio kwamba amejifunza kutokana na vitabu, bali kutoka moyoni mwake.

Baba Mtakatifu anasema kwamba mama kanisa naye hufanya hivyo hivyo kwa watotowake wa kiroho. Huwaonyesha njia na kuwalelea ili waweze kukua na kuishi vyema. Huku akiwaalika waliokuwa wakimsikiliza kufukiria juu ya Amri kumi, Baba Mtakatifu amesema kwamba amri hizo huonyesha njia ya kufuatwa ili kuweza kukua na kuwa na mwelekeo katika maisha. Nazo ni tunda la wema na mapendo makuu ambayo Mungu anawazawadisha watu wake.

Papa amewaalika watu wote kuziangalia amri hizo upya na sio kama amri au mambo yaliyokatazwa, bali kama viegemezo katika mahusiano yao na Mungu na binadamu wenzao.

Amri kumi za Mungu huwaalika waumini kujibandua na miungu ya uwongo, kuwaheshimu wazazi, wanyofu na waadilifu, na kuwaheshimu wengine. Haya ndiyo mambo ambayo mama humfunza mwanae ili aweze kuishi vyema, asema Baba Mtakatifu, na kwamba hakuna mama ambaye humfunza mtoto wake mambo mabaya kwani humtakia mema – kama ambavyo Kanisa linawatakia mema wanaye
.
Na hata mtoto akuapo na kushika njia zake mwenyewe, mama hendelea kumshauri na kumtegemeza ili aweze kujimudu katika hali zote, huku akiwa na saburi kuu, hata pale mtoto anapoonekana kuiacha njia aliyoonyeshwa na mama yake.

Kile kinachomsukuma Mama kufanya hivyo ni upendo, asema Baba Mtakatifu Francisko, na kwamba hata pale mtoto anapokosea mama huwa daima karibu na kumuonya kwa mapendo huku akiwa tayari kabisa kumsaidia kuirudia njia ifaayo.

Naye mama huwa daima tayari kuteseka kwa ajili ya watoto wake. Baba Mtakatifu amewaalika wote kuwafikiria hasa akina mama ambao watoto wao wamefungwa gerezani. Wamama hao bila woga wowote, huendelea kuwapenda watoto wao bila kujali kama wana hatia au la, huku wakikabiliana na hali ngumu zitokanazo na kejeli kutoka kwa jirani na marafiki. Hawaachi kamwe kujitoa kidete kwa ajili ya watoto wao.
Vivyo hiyo nalo Kanisa ni mama mwenye huruma kwa watoto wake na hutafuta njia za kuwasaidia daima hata kama wamekosea njia; hutafuta kuwatia moyo bila ya kuwahukumu. Hutoa msamaha wa Mungu hata kwa wale wanaojisikia kuwa kwenye giza kuu la dhambi. Baba Mtakatifu Francisko anawasifu akina mama kwa ujasiri wa kuwatakia na kuwaombea mema watoto wao, bila kuhesabu gharama.

Anasema baba Mtakatifu kwamba akina mama huwaombea hasa watoto wao walio dhaifu, walio na mahitaji ya kipekee, na wale walioasi. Ametoa mfano wa Mtakatifu Monica aliyemwombea mtoto Agostino. Kwenye siku ya mtakatifu Agostino hapo tarehe 28 mwezi Agosti 2013, Baba Mtakatifu alisali kwenye madhabahu ya Mtakatifu Monica iliyopo kwenye nyuba ya watawa wa Mtakatifu Agostino hapa mjini Roma, na ambapo yanahifadhiwa masalia ya mtakatifu huyo.

Baba Mtakatifu amewaomba akina mama wote kutochoka kuwaombea watoto wao kwa Mungu aliye na moyo mkuu na wa huruma. Amesema kwamba hata Mama Kanisa hachoki kuwaombea watoto wake wote katika kila hali ya maisha yao. Anawaalika wote kuunganisha sala zao na sala za Mama Kanisa anapowaonyesha wanae njia ya kufuata na kuwakabidhi mikononi mwa Mungu mwenyewe








All the contents on this site are copyrighted ©.