2013-09-11 15:36:28

Katekesi ya Papa - Kanisa ni mama tunayepaswa kumuenzi, kumpenda na kumlinda


Mapema Jumatano hii, Baba Mtakatifu Francisko, alitoa katekesi yake kwa mahujaji na wageni, hii ikiwa ni katekesi ya pili baada ya kipindi cha mapumziko ya wakati wa kiangazi. Mamia ya maelfu ya watu walikusanyika kumsikiliza Papa, watu waliotoka pande mbalimbali za dunia, Uingereza , Kenya, Italia, Marekani , na kwingineko , wote pamoja waliupamba uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro Vatican , kwa wingi wa rangi mbalimbali, wakiwa tayari kusikiliza mafundisho ya Papa.

Papa aliifungua katekesi yake, na wito wa kuitafakari sura ya Kanisa,katika mtazamo wa Maadhimisho ya mwaka wa Imani, na muono ulioelezwa na Mababa wa mwanzo wa kanisa na pia Mtaguso Mku wa pili wa Vatican , Kanisa, kama Mama wa waamini wa Kristu.

Alisema , "kwa hakika , Kanisa ni mama yetu katika imani , na maisha yaliyo juu ya uwezo wetu wa kibinamu , kama iliyotamkwa katika waraka wa Mwanga wa Mataifa “Lumen Gentium”. Ni sura iliyotajwa zaidi na Mababa wa Kanisa tangu karne za mwanzo wa kanisa".

Hivyo Papa anafikiri hata katika nyakati hizi zetu, ni muhimu kutambua hivyo na kuona haja ya kutafakari zaidi, ina maana gani na kwa namna gani Kanisa linakuwa Mama ?

Papa alilifafanua kanisa kama mama, akitaja vipengere vitatu .Kwanza Kanisa kama Mama, katika mtazamo wa mwanzo wa maishaya imani akifananisha mwanamke anavyoyabeba mimba tumboni mwake kwa miezi tisa, na kujifungua mtoto wake halisi, akiyafunua maisha mapya ulimwenguni. Hivyo kama ilivyo uzoefu huu wa kibinadamu kwa mama, kanisa pia hutupatia zawadi ya maisha tena maisha ya milele, kupitia utendaji w a Roho Mtakatifu. Roho tunayempokea kupitia sakramenti ya ubatizo , ambamo tunazaliwa upya kama watoto wa Mungu na kupokea maisha mapya. Pamoja na kwamba , imani ni utendaji wa mtu binafsi, lakini mtu hupata mang’amuzi hayo , kupitia wengine, katika familia zetu na jumuiya tunamoishi, tukiendelea kupata mafundisho na majiundo thabiti katika imani. Na hivyo familia inakuwa ni mama wa kwanza katika malezi ya kiroho. Kanisa kama ilivyo kwa mama zetu hutoa zawadi ya maisha.

Pili, Kanisa kama ilivyo kwa mama, hulisha watoto wake na kuwasaidia kukua , hufundisha njia inayofaa kupita na huwasindikiza katika mapito yote ya maisha na hasa wakati wa majaribu ya maradhi na dhiki , kupitia masakramenti na Neno la Mungu .

Tatu , Papa alikamilisha tafakari yake kwa kuelekeza mawazo katika karne za kwanza za kanisa , akisema, Kanisa lilikuwa wazi na halisi, kwamba ni Mama wa Wakristu wote. Na hivyo fikira na utendaji wa tangu mwazo wake unapaswa kuendelezwa nyakati zote bila ya kuwa na tofauti, hata katika nyakati hizi zetu. Hiiinakuwa na maana kwamba, ni wajibu wetu kama waamini , kusonga mbele katika kushirikishana umama huu wa kanisa, tukisaidiana na kutiana shime na nguvu za kuwaleta walio nje ya kanisa, katika maisha ya matakatifu ya imani kwa iliyofunuliwa na Mwenyewe kichwa cha Kanisa Yesu Kristu
.
Papa alimtaka kila muumini wa Kanisa, kujiuliza kama analipenda kanisa kama mama, anayemsaidia kukua katika ukomavu wa Mkristu. Na jinsi gani ya kusonga mbele na juhudi ya kuwaleta wengine katika upendo huu wa Kristu kwa watu wengine. Kama wana wa imani ndani ya Kanisa , ni wanao wajibu wao, kuifikisha nuru ya mwanga wa Kristu katika miisho yote ya dunia.

Baada ya Katekesi , Papa Francisko alisalimia kwa lugha mbalimbali kulingana na makundi yaliyokuwepo , wote akiwatakia amani ya Bwana Mfufuko, iandamane nao popote walipo, na kujazwa na upendo wa Kristu na kanisa lake, Mama Yetu.








All the contents on this site are copyrighted ©.