Mwombeni Mama Maria, Malkia wa Amani, kwa ajili ya amani dunian
Mama Kanisa anamheshimu mama Bikira Maria kama Malkia wa Amani. Naye baba Mtakatifu
Francisko, alipotoa mwito wa sala, mafungo na mkesha kwa ajili ya kuomba amani kwa
ajili ya Syri, Mashariki ya Kati na dunia nzima, aliuomba ulimwengu mzima umwangalie
Mama Maria kama mwombezi wa binadamu mbele yake Mwenyezi Mungu.
Hivyo siku
ya Jumamosi wakati wa kesha ya sala kwa ajili ya amani, Mama Bikira Maria alichukua
nafasi ya kipekee sana. Mbali na kusali Rozari Takatifu kwa pamoja, kulikuwepo pia
sanamu ya Bikira Maria inayoenziwa kama sanamu ya zamani zaidi katika historia ya
Kanisa.
Sanamu hiyo ijulikanayo kama Salus Populi Romani inahifadhiwa kwenye
madhabahu moja ndani ya Kanisa kuu la Maria Maggiore lililoko mjini Roma tangu mwaka
1611. Kuna tamaduni inayosadiki kwamba sanamu hiyo ilichorwa na Mtakatifu Luka. Hata
hivyo inaaminika kuwa ni mchoro wa karne ya 12, ambao unamwonyesha Maria akiwaelekeza
binadamu njia ya kufuata, Yesu Kristo.
Miujiza mingi imesemekana kutendeka
kutokana na sanamu hiyo kama ule wa karne ya Kumi na sita, pale mji wa Roma ulipokumbwa
na ugonjwa wa tauni, naye Baba Mtakatifu Pio V akaichukua sanamu hiyo kwenye maandamao
ya sala hadi Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro. Inasemekana kuwa kabla ya kulifikia Kanisa
hilo, wote waliokuwa kwenye maandamano hayo waliona kile walichokiita Malaika Mikaeli
kwenye mlima Adriani. Kutokana na muujiza huo Baba Mtakatifu alitabiri kuwa ile ilikuwa
ishara ya tauni kumalizika, na kweli, baada ya muda mfupi, iliisha kabisa. Kilima
hicho hata leo kinajulikana kama ngome ya Malaika Mtakatifu Mikaeli.
Mchoro
huo pia ulitumika kwenye maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani iliyofanyika Tor Vergata
Agosti, 2000 ambapo Baba Mtakatifu Yohanne Paolo II aliwakabithi vijana wote mikononi
mwa Mama Bikira Maria.
Baba Mtakatifu Francisko amewahi kusali mbele ya mchoro
huo mara kadhaa tangu kuchaguliwa kwake kama khalifa wa Mtakatifu Petro, kama vile
wakati wa kuanza mwezi wa rozari, Mei 2013, kabla ya kuelekea, na baada ya kurudi
kutoka Brazil kwenye maadhimisho ya Siku 28 ya Vijana duniani mwaka huu. Hii ni ishara
ya mapendo makubwa aliyo nayo Papa kwa Mama wa Mkombozi Yesu Kristo. Naye anawaalika
watu wote wa mapenzi mema kumtazama Mama huyu aliye Malkia wa Amani awezaye kuwaonyesha
njia ya amani kwa ajili ya Syria, Mashariki ya katin a dunia nzima.