2013-09-10 08:08:08

Mabavu na vita kamwe haviwezi kuleta amani!!!- Papa


Baba Mtakatifu Francisco Jumamosi jioni (07/09/ 2013) aliongoza ibada ya sala maalum kwa ajili ya kuwaombea amani waathirika wa migogoro na vita vinavoendelea nchini Syria, Mashariki ya Kati na kote duniani. Maelfu ya waumini na watu wenye mapenzi mema kutoka sehemu mbalimbali za dunia wamemiminika kwa wingi kwenye uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatikan, kusali pamoja na Baba Mtakatifu na Kanisa Katoliki, ishara ya mshikamano wa dunia nzima kwa ajili ya amani.

Wakati wa sala hizo Baba Mtakatifu amewaalika watu wote wenye mapenzi mema kuendeleza amani kpitia majadiliano, na msamaha. Amesema kwamba pale mwanadamu anapoanza kujifikiria yeye peke yake na maslahi yake binafsi, basi hufungua mlango wa migogoro na vita. Papa amemwalika kila mmoja kujichunguza ndani ya moyo wake kwani mwito wa amani ni wa kila mmoja.

Amesema kwamba Mungu aliuumba ulimwengu na kuona kwamba kila kilichokuwa ndani yake kilikuwa chema. Ni mwaliko kwa kila mtu kuyaona na kuyajali maslahi ya mwenzake kama ndugu wa kupendwa. Kwa kuwa na uhusiano wa kipekee na mwenyezi Mungu, kila mwanadamu anaweza kuyatajirisha mahusiano yake pia – yaani mahusiano na Mungu, na wengine na hata na nafsi yake mwenyewe - ili yaweze kuonyesha upendo, uaminifu, na wema utokanao na tafakari ya ndani ya moyo wake.

Baba Mtakatifu ametoa mwito kwa kila mwanadamu kuwa mlinzi wa mwenzake, huku akirejea tarajio la Mungu kwa Kaini kuhusiana na ndugu yake Habili. Mungu anamwuuliza Kaini: Yuko wapi ndugu yako, Habili? Naye Kaini anamuuliza Mungu: Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? (Mwanz 4:9).

Ni ombi la Papa Francisko kwamba watu wote, wanawake kwa wanaume, kote duniani, watayakumbatia maneno ya msamaha, mazungumzo na upatanisho, ili kuweza kujenga dunia yenye amani kwa mafao ya wote.











All the contents on this site are copyrighted ©.