2013-09-07 11:12:57

Makanisa Ulaya yaungana na Papa kuombea amani


Baraza la Mabaraza ya Makanisa ya Ulaya pamoja na Baraza la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya yamewaomba waumini wote wa ulaya kuungana pamoja na Baba Mtakatifu francisko kuombea amani Syria, Mashariki ya kati na kote duniani hapo siku ya Jumamosi (07/09/2013).

Mabaraza hayo pia yamewaalika viongozi wa mataifa 20, (G20) wanaoendelea na mkutano wao wa mwaka mjini Petersburg, Urusi , kujiunga na Askofu mkuu wa Kianglikani wa Canterbury, Justin Welby, na Baba Mtakatifu Francisco na viongozi wengine wa Kikanisa kufikiria kwanza njia ya majadiliano wala sio silaha, katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili dunia ya leo.

Kwenye ujumbe wa pamoja kuhusiana na migogoro na kinzani ya kivita inayoendelea nchini Syria, Mabaraza haya mawili ya makanisa ya Kikristo barani ulaya yanapinga aina yoyote ya vita na yanaonyesha mshikamano wao na wa makanisa ya ulaya na wakristo na watu wote wanaoendelea kuteseka nchini Syria kutokana na mauaji ya halaiki kwenye vita vinavyoendelea nchini humo.

Maaskofu hao wanasema kwamba amani ya kweli hutoka kwake mwenyezi Mungu na hivyo ni vyema kumwomba Mungu atujalie amani ndani ya mioyo yetu na kwa wale walioathirika na vita.

Ujumbe huo umewekwa sahihi na Kardinali Peter Erdò, Askofu Mkuu wa Esztergom, Budapest, aliye pia rais wa Baraza la mabaraza ya Maaskofu Katoliki, Ulaya; na Christopher Hill, Askofu wa Kianglikani wa Guildford, na rais wa Baraza la makanisa Ulaya.











All the contents on this site are copyrighted ©.