Uchumi wa kimataifa utaendelea kukua kama tu utafuata mfumo wenye kuyaheshimu na kuyajali
maisha na hadhi ya binadamu wote, kuanzia aliye mkubwa zaidi hata yule angalipo bado
tumboni mwa mama yake, sio tu kwa wananchi wanchi ishirini zenye uchumi mkubwa zaidi
duniani, lakini hata kwa kila mwananadunia, hata wale walio vijijini na wenye kusukumizwa
pembezoni mwa jamii.
Ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye barua aliyomuandikia
Rais Vladimir Putin wa Russia, ambaye pia ni rais wa mkutano mkuu wa nchi ishirini
zilizo na uchumi mkubwa zaidi duniani, (G20), zilizofanya mkutano wao wa mwaka, mjini
Petersburg, Urusi mwishoni mwa wiki (tarehe 05 na 06/06/2013) .
Kwenye barua
yake, Baba Mtakatifu Francisko alimkumbushia Rais Vladmir wajibu alio nao kwa kushehenewa
cheo cha urais wa mataifa hayo ishirini yenye uchumi mkubwa zaidi duniani, huku akisema
kwamba nchi ya Russia imehudhuria mikutano yote tangu mwanzo wa G20 na kwamba rais
huyo ameamua kuhakikisha kwamba biashara ya kimataifa itaendeshwa kistaarabu ili kuweza
kukabiliana na changamoto zinazoletwa na myumbo wa kiuchumi duniani.
Papa
alisema kwamba ni wazi kwamba migogoro na kinzani ya kivita inayoshuhudiwa sehemu
nyingi za dunia ni matokeo ya ubinafsi na kutotaka kuendeleza biashara na mahusiano
yenye kuchangia maendeleo endelevu na mafao ya wengi. Ni kukataa makusudi kutafuta
na kufuatia amani kwa kuendeleza mahusiano ya kibiashara yenye kuyaheshimu maisha
ya wengine; hivyo kusababisha mahangaiko, njaa, magonjwa na hata vifo kwa watu wengi
sana sehemu mbalimbali za dunia.
Anasema Baba Mtakatifu kwamba bila amani
haiwezekani kuwa na maendeleo ya kweli ya kiuchumi, na kwamba utumiaji wa mabavu kamwe
haujengi amani inayohitajika sana kwenye maendeleo ya kina.
Japo viongozi
hao wa mataifa ishirini yenye nguvu ya kiuchumi hawakuwa wanalenga kuzungumzia maswala
ya usalama duniani kwenye mkutano wao wa mwaka, Baba Mtakatifu aliwaalika kulimulikia
swala la Mashariki ya Kati na hasa Syria huku akisema alisikitika kwamba tangu mwanzo
wa migogoro ya Syria kumekuwa na kutokubaliana kwa ajili ya kupendelea upande fulani
fulani, hivyo kuongeza ugumu wa kutafuta suluhu ya amani nchini humo.
Baba
Mtakatifu alimwalika kila mmoja wa viongozi hao kusaidia kutafuta suluhisho la amani
na wala sio kwa njia ya utumiaji wa silaha, bali kwa majadiliano ambayo ndiyo yanayopendelewa
na jumuiya ya kimataifa, huku akiongezea kwamba serikali zote zinao wajibu wa kimaadili
kuwasaidia wenye kukumbwa na mahangaiko na mateso, hata nje ya mipaka ya nchi zao
wenyewe.