Katekesi ya Papa ya Jumatano: Vijana tumaini la kanisa na dunia
Vijana ni tumaini la Kanisa na dunia nzima na hivyo inawapasa kushiriki kikamilifu
kwenye shughuli zote za kikanisa na kijamii kwa ajili ya mafao ya watu wote. Ndiyo
changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko siku ya Jumatano hapa mjini Vatikan.
Baba Mtakatifu Francisco pia amemshukuru mwenyezi Mungu na wote waliofanikisha safari
yake nchini Brazil hivi karibuni ambapo aliweza kujumuika na mamilioni ya vijana kutoka
sehemu mbalimbali za dunia kwenye maadhimisho ya 28 ya siku ya vijana duniani.
Papa
ameirejea safari yake ya kichungaji nchini Brazil wakati wa Katekesi yake, Jumatano,
tarehe 4 Septemba 2013 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican,
uliokuwa umefurika kwa umati mkubwa wa waamini, mahujaji na watu wenye mapenzi mema.
Amesema
japo ni zaidi ya mwezi tangu akamilishe safari yake hiyo, lakini ameona umuhimu wa
kukumbushia yale yaliyotokea wakati wa maadhimisho hayo, akisema kwamba kwake yeye
aliye mzaliwa wa bara la Marekani ilikuwa zawadi kutoka kwa Mungu. Amemshukuru pia
Bibi Yetu wa Aparecida kwa ufanisi huo akisema kwamba Bikira Maria daima amekuwa kiini
cha imani Brazil. Amesema yeye binafsi, pamoja na ndugu zake maaskofu walishirikiana
kwa karibu kabisa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa Kumi na sita kwa kazi ya
kichungaji barani humo ambapo wanaishi wakristo wakatoliki wengi zaidi duniani.
Kwa
mara nyingine tena Baba Mtakatifu amewashukuru viongozi wa kidini na wale wa kiserikali,
mashirika ya kikatoliki na yale ya kiekumeni, makampuni na watu binafsi, maparokia
na miji na vijiji waliochangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha safari yake. Ni safari
ilyofanyika ndani ya mwaka wa imani ambamo pia Mama Kanisa anaadhimisha miaka hamsini
tangu Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikani.
Amewataja kuwa watu wa nguvu – WaBrazili
– kwa namna walivyoonyesha mambo maku matatu – Ukarimu, Sherehe na Umissionari.
Watu
wa Brazil walionyesha Ukarimu wao kwa Papa kwa namna walivompokea kwa moyo mkuu, moyo
mkunjufu na mapendo adili; Amesema papa kuwa siku ya vijana duniani ni sherehe kwa
wote kwani wakati vijana waliojaa furaha wanapofika kwenye mji fulani basi na wenyeji
pia hufurahi na kusheherekea pamoja nao. Ndivyo ilivyotokea hata na Brazil. Ila Brazil
kulikuwa na sherehe kubwa zaidi, sherehe ya imani, wakti kwa pamoja vijana na wasio
vijana waliungana kumsifu na kumtukuza Mungu, na kukesha huku wakilisikiliza neno
lake Mungu na kuyatafakari matendo makuu ya Mungu. Amesema Papa kuwa bila mapendo
ya kiMungu hakuwezi kuwa na karamu ya kikweli kati ya binadamu.
Mwishoni baba
Mtakatifu amesema kuwa moyo wa kimissionari ulijidhihirisha wazi kwenye sherehe za
maadhimisho ya Siku ya Vijana Brazil sanjari na maneno ya Kristo mwenyewe – E nendeni
mkayafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu. Baada ya kulisikiliza neno la Mungu
vijana walitumwa kulihubiri kote duniani.
Baba Mtakatifa aliwachangamotisha
vijana waliokuwa wanamsikiliza kwenye wuwanja wa kanisa Kuu la Mtakatifu Petro kuwa
wafuasi wa kristo akisema kwamba kwenye vijana kuna pia tumaini. Vijana nao walimshabikia
Baba Mtakatifu Francisko kwa vifijo na kushangilia kwa furaha pale alipowaomba kufungua
milango ya mioyo yao na kumwalika kristo na kuwa tumaini la Kanisa na dunia nzima.