2013-09-03 08:35:43

Papa aomba amani,ndani ya kila mtu na ulimwengu mzima


Baba Mtakatifu Francisko siku ya Jumapili (01.09.13) kwenye mahubiri yake ya wakati wa sala ya Malaika wa Bwana,sala iliyohudhuriwa halaiki kubwa ya watu kwenye uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro hapa mjini Vatican, aliomba amani, ndani ya kila mtu na katika ulimwengu mzima.

Amesema Papa Francisko kwamba anajisikia mmoja wa wale watu wote wanaotamani na kutafuta amani pote duniani. Kilio cha nguvu cha kuomba amani kinasikika kote ulimwenguni, alisema Baba Mtakatifu, wana dunia wanatamani amani, ndani ya mioyo yao, kwenye jamii na ulimwenguni kote. Hata hivyo inasikitisha kuona kwamba migogoro ya kila aina inaendelea kuvuruga amani kwenye maeneo mengi ya dunia. Anasema Baba Mtakatifu kwamba amani ni kitu cha thamani ya juu sana na kinapaswa kutafutwa kwa bidii na kukuzwa kwa bidii.

Baba Mtaklatifu alisema kwamba anaumia sana na kujaa masikitiko anapoona visa vingi vya vita na mivutano iliyomo kwenye dunia na hasa kwa siku za hivi karibuni. Amesema moyo wake u pamoja na watu wa Syria wanaokabiliwa na hali ngumu ya kivita.

Amewaomba watu wote kutoka ndani ya mioyo yao, kukuza amani kwani migororo inasababisha mateso mengi na watu wengi kukata tamaa ya maisha. Amelaani vitendo vya utumiaji wa silaha za kemikali dhidi ya wanachi wa Syria, kitendo ambacho kimesababisha vifo vya watu wengi na kimeshtua dunia nzima. Anasikitishwa pia na maumivu na mateso wanayoyapata wananchi wasio na silaha, na idadi ya watoto wengi wa Syria wanaopoteza maisha yao kwenye ghasia hizo na hivyo kukosa fursa ya kuyaona maisha yambeleni.

Baba Mtakatifu amewasihi wapiganaji wote kukisikiliza kilio cha roho zao wenyewe na waache kuyatafuta maslahi yao binafsi, bali wamwone kila mtu kama dada au kaka yao wenyewe hasa na hivyo waamue kiujasiri kutafuta suluhisho la migogoro yao kwa njia ya mazungumzo na makubaliano na waache misimamo mikali ambayo inawafanya kuwa vipofu machoni mwa mateso ya ndugu zao.

Wakati huohuo ameiomba jumuiya ya kimataifa kufanya juhudi zote ili kuongoza majadiliano na makubaliano yatakayoiletea nchi ya Syria na watu wake amani ya kudumu kwa manufaa ya kila mmoja.

Ameyaomba pia mashirika ya misaada kuhakikisha yanatoa msaada wa kutosha kwa wana Syria ili kuweza kupunguza maumivu wanayoyapitia kwa wakati huu.

Baba Mtakatifu amewachangamotisha wote waliokuwa wanamsikiliza kuona kwamba kila mmoja ana mchango katika kuleta amani kwenye jamii yake na duniani kwa ujumla. Kujifunza kuishi kwa mapendo na kuvumiliana kidugu ndio siri ya kudumisha amani, amesema Papa huku akiinukulu hati ya kichungaji yamwaka 1963, Pacem in Terris au Amani duniani iliyokuwa mchango wa mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vaticani.

Baba Mtakatifu amesema kuwa watu wote wanaunganishwa na jukumu moja la kuendeleza amani, Wakatoliki hata wasio wakatoliki, wakristo na wasio wakristu, na hata wale wasioamini diini yoyote, na kwamba amani ni tunu yenye kuvunja utengano wa aina yoyote kwani ni urithi wa binadamu wote kwa ujumla; huku akiwatahadharisha watu wote kwamba utamaduni wa kutumia nguvu au migogoro hausaidii kujenga mahusiano mema kati ya jamii ila utamaduni wa mawasiliano ndiyo njia muafaka ya kuleta amani.











All the contents on this site are copyrighted ©.