Kardinali Oscar Andrès Rodriguez Maradiaga, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada
ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, atazuru Kanisa la Canada wakati
wa Mkutano Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa nchi hiyo utakaofanyika kuanzia tarehe 23
hadi 27, Septemba 2013.
Kardinali huyo kutoka Honduras ni mmoja wa washauri
8 walioteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya mageuzi nchini Vatican atahutubia
mkutano huo juu ya mada ya Jukumu la Maaskofu katika kuendeleza haki, amani na mapendo.
Nao Maaskofu wa Canada watachukua fursa hiyo kuchambua kwa kina miaka 50 tangu
Baba Mtakatifu Yohane wa 23 alipochapisha hati ya kichungaji Pacem in Terris – Amani
Duniani mnamo mwaka 1963 kama moja ya mapendekezo ya mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili
wa Vatikani. Mama Kanisa anapoendelea kuadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 50 tangu Mwenyeheri
Yohane XXIII alipochapisha Waraka huo wa kichungaji, Pacem in Terris, Amani Duniani,
ni changamoto kwa wote kuendelea kuithamini amani kama tunu inayowaunganisha wanadamu
wote.
Kardinali Maradiaga pamoja na Maaskofu wa Canada watatumia pia mkutano
wa tarehe 23 hadi 27 Septemba 2013 kama wakati muafaka kwa kutafakari juu ya changamoto
na mabadiliko ya uongozi wa kanisa nchini humo.