Kanisa barani Afrika na kote duniani linaungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia
kuomboleza kifo cha aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Lusaka, Kardinali Medardo
Joseph Mazombwe, aliyefariki dunia siku ya Alhamisi (29.08.2013) kwenye hospitali
ya Chuo Kikuu cha Ukufunzi cha Lusaka. Kardinali Mazombwe alizaliwa kunako tarehe
24 Septemba 1931 kwenye kitongoji cha Katete kilichoko Mashariki mwa Zambia. Alipewa
daraja ya Upadri tarehe 4 Septemba 1960 na hatimaye kuteuliwa kuwa Askofu wa jimbo
la Chipata mnamo tarehe 7 Februari 1971. Cardinali Mazombwe alihudumu kama Askofu
Mkuu wa Jimbo Kuu la Lusaka kuanzia mwaka 1996 hadi kustaafu kwake hapo mwaka 2006.
Tarehe 30 mwezi Novemba 2010 Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa Kumi na sita
kwenye kikao cha hadhara katika Basilika ya Mtakatifu Petro mjini Vatican, alimteua
Askofu Joseph Mazombwe kuwa Kardinali wa kwanza mwenyeji wa Zambia. Mama Kanisa
atamkumbuka Kardinali Mazombwe kwa mchango wake mkubwa kupitia huduma mbalimbali ndani
na nje ya Kanisa. Itakumbukwa kwamba katika uhai wake, Kardinali Mazombwe amehudumu
kwenye nafasi muhimu mbalimbali. Kwa vipindi vitatu vya miaka mitatu mitatu, Kardinali
Joseph Mazombwe aliwahi kuchaguliwa kama rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia,
na pia kuhudumu kama Mwenyekiti wa Baraza la Mabaraza ya Maskofu Katoliki Afrika Mashariki
na ya Kati (AMECEA) tangu 1979 hadi 1986. Kwenya matayarisho ya kuadhimisha jubilee
ya miaka 2000 ya ukristu, Kardinali Mazombwe, akiwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Lusaka
alishiriki kikamilifu kwenye kampeni ya kuiomba jumuiya ya kimataifa kufutilia mbali
deni la kimataifa la nchi yake ya Zambia. Zambia na mataifa mengi duniani yalijiunga
na kampeni hiyo ya kimataifa kama tendo la kuuunga mkono mwito wa aliyekuwa Baba Mtakatifu
Yohani Paulo II kwa jumuiya ya kimataifa kuonesha mshikamano na nchi nyingi zinazoendelea
na zinazojitahidi kujitoa kwenye umaskini usio na kifani, lakini zinajipata zikiendelea
kusongwa na uzito wa madeni kimataifa. Kanisa la Zambia pia litamkumbuka Cardinal
Mazombwe kwa mchango wake wa kichungaji na kujitoa bila ya kujibakiza na hasa katika
kujenga Kanisa Kuu la Mtoto Yesu lililoko mjini Lusaka. Kardinal Mazombwe pia atakumbukwa
kwa ujasiri na moyo wa matumaini hata katika kukabiliana na ugonjwa wa saratani ambao
aliupokea kwa moyo wa imani kuu. Mungu aiweke roho yake Kardinal M. Joseph Mazombwe
mahali pema mbinguni.