Mitandao ya kijamii: Milango ya ukweli na imani, uwanja mpya wa uinjilishaji
Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika Kusini litaadhimisha Jumapili ya mawasiliano ya
kijamii siku ya Jumapili ya tarehe 1 Septemba 2013. Mada ya maadhimisho hayo itakuwa
Mitandao ya kijamii: Milango ya ukweli na imani, uwanja mpya wa uinjilishaji.
Maaskofi
Katoliki nchini Afrika Kusini wamechangamotishwa na mada ya siku ya mawasiliano duniani
juu ya mitandao ya kijamii iliyotolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi
na sita. Maaskofu hawa wa Afrika Kusini wamewaandikia barua waumini wote nchini humo
kushiriki kwenye maadhimisho ya siku ya mawasiliano nchini humo hapo siku ya Jumapili
(01.09.2013).
Maaskofu hao wamesema kwamba Baba Mtakatifu anawaalika wote kutumia
mitandao ya kijamii kwa ajili ya uinjilishaji na hivyo jamii ya waumini haina budi
kuandaa washa na semina kwa ajili ya mafunzo juu ya utumiaji muafaka wa mitandao hiyo.
Makanisa na Parokia hayana budi kuchagua mitandao inayofaa na kuitumia kwa
ajili ya manufaa ya jamii kwa ujumla, wakizingatia maswala ya kisheria, kimaadili
na kiroho hata katika utumiaji huo ili kuweza kufanya uinjilishaji muafaka kwa kizazi
kipya.
Maaskofu hawa pia wamewachangamotisha waumini kuchambua njia wanazotumia
katika kuwasiliana kwenye maparokia na kuhakikisha kupyaisha njia zote za mawasiliano
ili kuweza kuliendeleza kanisa nchini humo.