2013-08-27 11:06:35

Zingatieni maadili, ukweli na uwazi katika masuala ya biashara


Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani hivi karibuni, akizungumza kwenye mkutano wa kwanza wa kimataifa kwa ajili ya wakurugenzi wa Kikatoliki kutoka Barani Afrika (UNIAPAC) uliofanyika mjini Yaoundè nchini Cameroon, aliwataka wakurugenzi hao kuhakikisha kwamba, wanazingatia misingi ya maadili, ukweli na uwazi wanapotekeleza wajibu wao kwa umma.

Hii ni changamoto ya kuondokana na uchu wa mali na tamaa ya faida kubwa ambayo imepelekea baadhi ya makampuni na mashirika kujikuta kwamba, yanakiuka misingi ya maadili kwa kisingizio cha kupata faida kubwa. Kardinali Turkson anasema, utekelezaji wa maadili unaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa faida katika makampuni na mashirika hayo.

Kardinali Turkson aliwasilisha pia salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na kuendelea kufafanua jinsi ambavyo Kanisa Katoliki linapenda kuchangia katika masuala mbali mbali ya kiuchumi, hasa wakati huu ambako watu wengi wanaendelea kuathirika na myumbo wa uchumi kimataifa, kwa kukazia sheria na kanuni maadili, ili kila mdau aweze kuchangia kadiri ya uwezo wake katika mchakato wa kufufua uchumi, kwa ajili ya mafao ya ustawi wa wengi.

Kama wakurugenzi wa makampuni na mashirika mbali mbali kutoka Barani Afrika, wanao wajibu mkubwa kwa Jumuiya zao. Ni rahisi sana kwa wakurugenzi ha ona makampuni yao kuvutwa na mantiki ya soko inayowasukuma kutafuta faida kubwa kwa gharama yoyote, kiasi kwamba, wakati mwingine kanuni na sheria maadili zinawekwa pembeni. Kama wasimamizi wakuu wanapaswa kuangalia ustawi na maendeleo ya wafanyakazi wao, kwa kuwatendea haki na kuwapatia mishahara inayokidhi mahitaji yao msingi.

Lakini, mantiki inayotawala soko huria katika uchumi ni tabia ya kuwanyonya na kuwadhalilisha wafanyakazi ili kujipatia faida kubwa, jambo ambalo ni hatari na chanzo cha kinzani na migomo katika Jamii. Wafanyakazi wakithaminiwa na kuheshimiwa, wakapatiwa haki zao msingi, watajenga ndani mwao moyo wa sadaka na majitoleo ambayo yanaweza kuwa ni kichochea cha uzalishaji mkubwa, tija na mafanikio.

Wafanyakazi wahamasishwe kujenga moyo wa kujitoa sadaka kwa kutendewa haki na kamwe makampuni na mashirika yasikimbilie kupata faida kubwa kwa gharama ya wafanyakazi wake. Kama wakurugenzi wanayo dhamana ya kutafuta kwanza kabisa mafao ya wengi badala ya kumezwa na uchu wa mali na faida kubwa kwa ajili ya kikundi cha watu wachache katika Jamii.

Waamini kwa namna ya pekee, wanachangamotishwa kutolea ushuhuda wa imani yao katika matendo wanapotekeleza majukumu yao ndani ya Jamii. Kwa maneno mengine, wanahamasishwa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao adili mbele ya Mungu na jirani wanaokutana nao kila siku wakati wa kazi. Hapa kuna haja ya kumwilisha imani katika matendo ya kila siku, ili kuondokana na uchu wa mali ambao umewatumbukiza wengi katika dibwi la rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma.

Kardinali Turkson anasema, kama viongozi wa mashirika na makumpuni katika nchi zao, wanahamasishwa kujenga umoja na mshikamano na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, wale ambao hawakubahatika kupata utajiri kama wao, kwa kuwasaidia. Watambue kwamba, kuna umati mkubwa wa watu unaoteseka kutokana na ujinga, umaskini na magonjwa na hapo hapo kuna kundi la watu wachache linaloendelea kufaidi matunda ya uhuru kwa kujibovusha mno kwa kupenda anasa na starehe kupita kifani.

Kardinali Turkson anasema, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwahamasisha waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema utajiri wa mali na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mafao ya wengi, ustawi na maendeleo ya jirani zao. Ni changamoto ya kuachana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine na badala yake kuanza kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa mshikamano wa umoja na upendo kama ndugu.

Mwelekeo huu si rahisi kuweza kuumwilisha katika uhalisia wa maisha, kwani uchu wa mali na faida kubwa ni kati ya mambo yanayoendelea kupewa msukumo wa kwanza kwa watu wengi ndani ya Jamii. Lakini, Kanisa bado linawachangamotisha watu kujitahidi kuvunjilia mbali kuta za utengano kati ya maskini na matajiri wa kupindukia hali inayochangia pia rushwa na ufisadi. Mambo haya kwa sasa ni chanzo cha kinzani na migogoro mingi ya kijamii na matokeo yake sheria zinapindishwa kwa sababu ya utajiri wa baadhi ya watu ndani ya Jamii.

Watu wajenge ari na moyo wa matumizi bora ya rasilimali: fedha na watu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Kiongozi na mfuasi safi wa Kristo anapaswa kutekeleza wajibu wake kwa kutambua kwanza kabisa kwamba, uongozi ni huduma inaosimikwa katika misingi ya haki na amani.

Mihimili hii ikizingatiwa kwa dhati kabisa anasema Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani watu wataweza kupata mali ya halali inayotoa huduma bora kwa jamii pamoja na kuwasaidia maskini; pili, makampuni na mashirika yao yatakuwa ni fursa za ajira kwa makundi makubwa ya vijana wanaotangatanga wakitafuta riziki yao ya kila siku na hivyo utu na heshima yao vitaweza kudumishwa na mwishowe, utajiri na mafanikio yanayopatikana yatasaidia kulinda na kutunza mazingira na watu wanaoishi katika maeneo haya.
All the contents on this site are copyrighted ©.