Wabunge Wakatoliki kukutana na Papa Francisko mjini Vatican
Wabunge Wakatoliki kutoka Kenya wako mjini Roma nchini italia kwa madhumuni ya kuhudhuria
warsha ya kimataifa kwa ajili ya Wabunge Wakatoliki. Habari iliyochapishwa kwenye
jarida la Star la Kenya inasema kwamba, madhumuni ya mkutano huo mjini Roma ni kutafakari
na kupanga mikakati ili kuhakikisha siasa zinaoana na mpango wa Mungu kwa watu wake.
Katika mahojiano na jarida la The Star, Makamu Mwenyekiti wa Wabunge wakatoliki
nchini Kenya, Bwana Chris Wamalwa, anasema kwamba wakiwa mjini Roma watamtembelea
pia Baba Mtakatifu Francisko kwenye Ikulu ya Vatican. Wabunge hao watapata fursa
ya kukutana na kujadiliana na wenzao kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Bwana
Chris Wamalwa amechukua uongozi wa kundi la wabunge wakatoliki nchini Kenya hivi karibuni
kutoka kwa aliyekuwa makamu wa kundi hilo, John Mututho.