2013-08-27 12:47:07

Mshikamano wa Maaskofu na waathirika wa machafuko ya kisiasa nchini Misri


Marekani haina budi kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa ili kuuunga mkono juhudi zinazofanywa na wananchi wa Misri ili kumaliza migogoro na malumbano ya kivita na kurejesha amani na utawala wa kisheria nchini Misri.

Ni maneno ya Askofu Richard Pates, Mwenyekiti wa kamati ya Haki na Amani Kimataifa ya Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani kwenye barua aliyomwandikia Katibu wa Serikali ya Marekani Bwana John Kerry hivi karibuni. Kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano na msamaha ili kudumisha misingi ya haki, amani na uhuru wa kidini nchini Misri.

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linasikitishwa na hali ya Misri na pia linalaani mwelekeo uliochukuliwa na baadhi ya wananchi wa Misri kushambulia Makanisa na miundo mbinu ya huduma za kijamii. Maaskofu wanaungana na Baba Mtakatifu Francisko ili kuiombea Misri, waathirika na familia zao na watu wote wanaoendelea kuteseka kutokana na misukosuko nchini Misri.

Maaskofu wanawashukuru na kuwapongeza wananchi wa Misri walionesha uungwana kwa kutetea mali ya Kanisa dhidi ya mashambulizi. Waathirika wakuu wa machafuko na migogoro kama hii ni maskini, wanawake na watoto!

Shirika la Misaada la Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, CRS linashirikiana na Kanisa la Misri katika jitihada za kuwasaidia waathirika wa vurugu na kinzani nchini Misri.
All the contents on this site are copyrighted ©.