2013-08-27 14:47:02

Mchango wa wanawake Barani Afrika!


Zaidi ya wanawake Wakatoliki 6000 wamehudhuria Semina ya kumi kimataifa kwa ajili ya Wanawake Wakatoliki. Semina hiyo imefanyika hivi karibuni mjini Cotonou, Benin, na kuyahusisha mataifa ya Benin, Togo, Ghana, Nigeria, Niger, Burkina Fasso, Senegal na Pwani ya Pembe. Wanawake hao wametumia muda wao wa sala, tafakari, na kuabudu Ekaristi takatifu ili kuangalia dhamana, wajibu na changamoto zinazowakabili wanawake Barani Afrika.
Mama Kanisa anaendelea kuthamini mchango unaotolewa na wanawake ndani na nje ya Kanisa, kama anavyobainisha Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita kwenye hati yake ya kichungaji Africae Munus au Dhamana ya Afrika, iliyochapishwa hapo 2011, anapoandika kwamba “wanawake wa Afrika, kwenye familia, jamii na Kanisa kwa kutumia talanta na vipaji walivyojaliwa” na kwamba wao ni kama uti wa mgongo wa Makanisa mahalia kwani wanashiriki na kujitoa bila ya kujibakiza kwenye maisha ya kichungaji ya Kanisa kupitia mashirika na vyama mbali mbali vya kichungaji kwenye Parokia na majimbo yao.
Mkutano wa Cotonou umetoa huduma ya Uinjilishaji kwa wanawake ili waendelee kutoa mchango wao wa hali na mali kama wanawake na waalimu ndani ya Jamii na Kanisa na hasa katika kuchangia maendeleo na ustawi wa Bara la Afika. Haya yote yatawezekana tu ikiwa kama Neno la Mungu litakuwa ni dira ya shughuli za wanawake wa Afrika hasa wakati huu ambapo Bara la Afrika linakumbwa na changamoto mbalimbali.
Naye Askofu Mkuu Brian Udaigwe, Balozi wa Vatican nchini Benin, katika ujumbe wake kwa Wanawake Wakatoliki waliokusanyika mjini Cotonou anasema kwamba, kuna umuhimu kwa wanawake kwa wanaume, kumsikiliza kwa makini zaidi Kristo na kuwa na mwamko mpya katika mchakato wa Uinjilishaji mpya ili kumshuhudia kwa ujasiri zaidi Kristo na ujumbe wa Injili inayosimikwa katika amani, upendo na mshikamano wa dhati.
Ni wakati muafaka kwa Wanawake Wakatoliki, watakakatifu waliojazwa na Roho Mtakatifu na wenye ujasiri wa imani, kuwa mstari wa mbele kuusaidia ulimwengu wa leo unaosukwasukwa na changamoto za utandawazi, anasema Askofu mkuu Udaigwe.
Naye Askofu Mkuu mstaafu Antoine Ganyè wa Jimbo kuu la Cotonou, Benin, amewaomba waliohudhuria mkutano huo kumwangalia Mama Bikira Maria aliyeongozwa na imani, na wala sio fikira za kibinadamu, kumpokea na kumlea Kristo Masiha.
Itakumbukwa kwamba, Wanawake wamekuwa mstari wa mbele kuhusiana na mambo ya imani, kama ilivyobainika kwenye mkutano huu uliotambua mchango na wajibu wa wanawake kama waalimu wa sala kwenye familia, waenezaji wa amani na upatanisho; mashahidi kwenye makazi na maeneo ya shughuli zao za kila siku; wahamasishaji wa maadili ya Kikristo na hata mfano wa kuigwa katika kuziishi heri za kiinjili na maisha ya kitawa.
Wamesema wanawake hao kuwa hawana shaka kwamba Roho wa Mungu yu juu yao na ataendelea kuwaimarisha na kuwahuisha ili kushiriki kikamilifu kwenye shughuli zote za Uinjilishaji mpya na kuyapyaisha maisha sio tu ya Barani la Afrika bali hata nje ya Bara la Afrika.

Imehaririwa na Sr. Bridgita Samba Mwawasi kutoka Gazeti la L’Osservatore Romano










All the contents on this site are copyrighted ©.