Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, aliutangaza na kuuzindua Mwaka wa
Imani sanjari na Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Miaka 20
tangu Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili alipochapisha Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki.
Lengo kuu la Mwaka huu ni kuwawezesha waamini kuifahamu kwa kina Imani wanayokiri;
Imani inayoadhimishwa katika Sakramenti za Kanisa; hii ndiyo Imani inayopaswa kuwa
ni dira na mwongozo wa maisha adili yanayofumbata Amri Kumi za Mungu. Mwishoni, hii
ni Imani ambayo inajidhihirisha kwa namna ya pekee katika maisha ya Sala inayomwilishwa
katika uhalisia wa maisha, ili kujenga na kuimarisha uhusiano wa dhati na Mwenyezi
Mungu.
Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Kardinali Zen Ze-kiun, Askofu
mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Hong Kong, China amekuwa akiendesha Katekesi za kina
kama sehemu ya mchango wa ushuhuda wa imani yake kwa Kristo na Kanisa lake. Katekesi
hizi kwa sasa zitasambazwa kwa njia ya DVD na CD kwa ajili ya matumizi ya Waamini
wa Kanisa Katoliki nchini China.
Hizi ni Katekesi zilizokuwa zinahudhuriwa
na umati mkubwa wa waamini na watu wenye mapenzi mema waliokuwa wanakiu ya kutaka
kufahamu kuhusu: Imani, Sakramenti za Kanisa, Amri za Mungu na Maisha ya Sala; mambo
ambayo yamefafanuliwa kwa kina na mapana kwenye Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki,
utajiri na urithi mkubwa kutoka kwa Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, Matunda ya Mtaguso
Mkuu wa Pili wa Vatican, kama zilivyo Sheria za Kanisa. Katekesi hizi pia zimeanza
kusambazwa kwa njia ya mitandao, ili kuwawezesha waamini walioko mbali zaidi kuweza
kujitajirisha katika imani kwa Kristo na Kanisa lake.
Kardinali Zen Ze-kiun
anasema, sehemu ya kwanza ya Katekesi hizi ambayo tayari inafanyiwa kazi ili kuwekwa
kwenye DVD inagusia: Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Hii ni changamoto iliyoibuliwa na
waamini waliotaka kufahamu kwa kina Imani yao kwa Kristo na Kanisa lake katika Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani, kwani hii ni sehemu ya majiundo endelevu.
Ni kweli waamini
walipokuwa wanapokea Sakramenti mbali mbali za Kanisa walipewa mafundisho, lakini
kuna haja ya kuanzisha mchakato wa majiundo endelevu, ili kuimarisha na kukomaza imani
miongoni mwa waamini, tayari kuweza kuitolea ushuhuda katika maisha yao yak ila siku.
Huu ndio umuhimu wa imani tendaji, changamoto inayotolewa na Mama Kanisa katika Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani.
Kardinali Zen Ze-kiun anasema Maadhimisho ya Mwaka wa Imani
sanjari na Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican imekuwa ni fursa
kubwa kwa waamini kujitajirisha kwa nyaraka mbali mbali zilizotolewa na Mababa wa
Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu
mamboleo.
Vyama vya kitume vimeendelea kutoa Katekesi maalum kuhusu utume
na dhamana yao katika Kanisa na mwaliko wa kuendelea kuyatakatifuza malimwengu kwa
njia ya ushuhuda wa maisha adili. Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa hasa Ubatizo
wakati wa Kipindi cha Pasaka, Kanisa linaendelea kukazia umuhimu wa majiundo makini
kwa Wakatekumeni ili waweze kuifahamu imani watakayoiungama, adhimisha, ishi na kusali.
Mwaka wa Imani, kimekuwa ni kipindi cha kukuza na kuendeleza utume wa Biblia
uliowahusisha Makleri, Watawa na Waamini walei ambao wamebobea katika Maandiko Matakatifu,
yote haya yanalenga anasema Kardinali Zen Ze-kiun kuwaimarisha waamini katika hija
ya maisha yao ya imani.
Alipokuwa mjini Vatican, alipata fursa ya kuzungumza
na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita kuhusu Katekesi za kina kama sehemu
ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto alifurahishwa sana
na jitihada hizi zinazolenga kuwaimarisha waamini katika imani yao kwa Kristo na Kanisa
lake, ili waweze kuwa tayari kuitolea ushuhuda.
Alipobahatika kuzungumza na
Papa Francisko, alimwelezea pia mikakati ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani nchini China.
Anasema, alikuwa anafahamiana kwa karibu na Kardinali Bergoglio kwani walikuwa ni
wajumbe wa Tume ya Sinodi ya Ekaristi iliyokusanya matunda ya Sinodi hiyo na kwamba,
walishiriki kwa pamoja kuandaa Sinodi zilizofuatia pamoja na kukutana mara kwa mara
wakati wa mikutano elekezi ya Makardinali wakati wa “Conclave” iliyopita mjini Vatican.
Anasema Makardinali walipokuwa wamekusanyika kwa ajili ya kumshukuru na kumuaga
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, alibahatika kukaa karibu na Kardinali
Berglio ambaye alimshirikisha maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini China. Kardinali
Berglio alisikiliza kwa makini. Kardinali Zen Ze-kiun anasema, kwa hakika Baba Mtakatifu
Francisko ni kiongozi anayetoa kipaumbele cha kwanza katika mikakati ya kichungaji
na ana kipaji kikubwa cha kusikiliza kwa makini.