Mama Kanisa anahitaji kuibua mbinu, mikakati na sera mpya zaidi katika ulimwengu wa
mawasiliano ya jamii ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo ya sayansi
na teknolojia katika ulimwengu wa mawasiliano. Kanisa halina budi kutambua dhamana
na nafasi yake katika Jamii husika, hii ndiyo changamoto iliyopo kwa sasa.
Ni
maneno ya Monsinyo Paul Tighe, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii
anapotafakari dhamana na utume wa Kanisa katika ulimwengu wa mitandao ya kijamii yenye
fursa na changamoto zake. Mawasiliano hayana budi kuangaliwa katika mapana yake kiulimwengu,
lakini ikumbukwe kwamba, yanagusa pia undani wa maisha ya watu mahalia.
Kanisa
linapaswa kuibua mmbinu mkakati ambao utayasaidia Makanisa mahalia kuwepo kwenye mitandao
ya kijamii kwa ajili ya waamini na watu wao mahalia pamoja na kuendelea kushiriki
katika maisha na utume wa Kanisa la kiulimwengu. Dhana hii inahitaji majitoleo na
ugunduzi utakaoiwezesha Injili kujikita katika mitandao ya kijamii, ili waamini na
watu wenye mapenzi mema, waweze kushirikishana mang’amuzi ya kweli za Kiinjili.
Monsinyo
Paul Tighe anasema, hizi kati ya mada zitakazojadiliwa na wajumbe wa Baraza la Kipapa
la Mawasiliano ya Kijamii katika mkutano wake wa Mwaka unaotarajiwa kuanza hapo tarehe
19 hadi tarehe 21 Septemba 2013 hapa mjini Roma. Kanisa linaendelea kujifunza matumizi
ya mitandao mipya ya kijamii kama ilivyojitokeza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya
28 ya Vijana Duniani mjini Rio de Janeiro, Brazil. Njia hizi mpya pengine ni mpya
kwa wale wanaoanza kuzitumia, lakini kwa vijana wa kizazi kipya, mitandao hii imekuwa
ni sawa na maji kwa glasi.
Ni mitandao inayowashirikisha na kuwagusa watu wengi
kwa pamoja, kiasi kwamba, hata wale wanaoishi pembezoni mwa Jamii wanaweza kupokea
ujumbe huu pasi na mashaka. Ujumbe unaotolewa na Mama Kanisa katika mazingira kama
haya hauna budi kuandaliwa kikamilifu ili kupata matunda yanayokusudiwa. Ni ujumbe
unaotoka moja kwa moja kwa viongozi wa Kanisa ambao wakati mwingine inakuwa ni vigumu
kupokelewa na wahusika katika maeneo yao, kwani hauwagusi moja kwa moja.
Monsinyo
Paul Tighe anasema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ana lugha rahisi inayowagusa watu
kwa haraka zaidi; ni kiongozi anayetumia vitendo kama ushuhuda wa kile anachozungumza.
Maneno na matendo ni chanda na pete katika kuwasilisha ujumbe unaokusudiwa na hapa
Baba Mtakatifu Francisko ameonesha umahiri mkubwa. Katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana
Duniani kwa Mwaka 2013, Baraza la Kipapa la Mawasiliano lilitumia mbinu mbali mbali
ili kuhakikisha kwamba, vijana wengi zaidi wanapata ujumbe kutoka kwa Baba Mtakatifu
Francisko.
Mtandao wa Vatican unaendelea kuboreshwa zaidi kwani kwa sasa watumiaji
wa mtandao huu wanaweza kupata: Gazeti la L’Osservatore Romano, Kusikiliza Radio Vatican
na kuona picha zinazorushwa na Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV pamoja na kujisomea
nyaraka na makala mbali mbali kuhusu maisha na utume wa Kanisa. Sasa hivi nyaraka
hizi zinawafikia watu wengi zaidi kwa njia ya mitandao ya kijamii na simu za viganjani.
Maelfu
ya vijana wameweza kupata ujumbe wa Baba Mtakatifu wakati wa Maadhimisho ya Siku ya
Vijana Duniani kwa njia ya mitandao ya Kijamii na hasa zaidi kwa njia ya simu za kisasa.
Huu ni ushirikiano wa dhati uliooneshwa na makampuni ya simu kutoka sehemu mbali mbali
za dunia. Vijana wameshirikishana picha na ujumbe kwa njia ya simu na mitandao mingine
ya kijamii kama vile twitter.
Monsinyo Paul Tighe anasema, wafuasi wa Baba
Mtakatifu Francisko katika mtandao wake wa twitter wamefikia millioni nane, na kwamba,
Baba Mtakatifu Francisko ni kati ya viongozi mashuhuri duniani ambaye ujumbe wake
unatafutwa ili kuwashirikisha wengine.
Huu ndio umuhimu wa kuwahusisha waamini
kuwa ni wasambazaji wa ujumbe wa Baba Mtakatifu, lakini zaidi Injili ya Kristo kwa
wajuani wao, ili kujenga jukwaa la majadiliano na ufahamu wa kina, ili kueneza Imani
na kweli za Kiinjili kwa watu wenye kiu na njaa ya Neno la Mungu. Kwa njia hii, Kanisa
linaweza kuonesha uwepo wake katika maisha ya watu kwa njia ya mitandao ya kijamii.
Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 yamekuwa ni kati ya matukio
yaliyofuatiliwa na watu wengi zake kwa mwaka huu kadiri ya takwimu zilizotolewa na
watumiaji mbali mbali wa mitandao.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi
na sita, katika ujumbe wake kwa Siku ya Upashanaji Habari Duniani kwa Mwaka 2013 aliwataka
waamini kujishughulisha kikamilifu katika mchakato wa kuwamegea wengine: Imani na
kweli za Kiinjili kwa njia ya uwepo wao kwenye mitandao ya Kijamii, ili kujadiliana
na kushirikishana utamu na uzuri wa Injili.
Baraza la Kipapa la Mawasiliano,
litatumia mkutano mkuu kujadili mafanikio na mapungufu yaliyojitokeza katika mawasiliano
ili kujiwekea mbinu mkakati wa maboresho kwa siku zijazo. Ni fursa ya kuangalia changamoto
na kiu inayooneshwa na watumiaji wa mitandao ya kijamii. Ni nafasi ya kusikiliza yale
yaliyojadiliwa ili kugundua kwa namna ya pekee: matumaini, furaha na machungu yanayomsibu
binadamu katika ulimwengu mamboleo na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Hii
inaonesha kwamba, kimsingi Kanisa linasikiliza na linapania kujenga jukwaa la majadiliano
ili kutoa ushuhuda wa Kiinjili, ndivyo anavyohitimisha tafakari yake Monsinyo Paul
Tighe, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii. Imehaririwa na
Padre Richard Mjigwa, C.PP.S. Idhaaya Kiswahili ya Radio Vatican.