2013-08-26 13:50:12

Papa alilia vita ya syria isitishwe.

Jumapili wakati wa adhuhuri, akiongoza sala ya Malaika wa Bwana mbele ya umati mkubwa wa mahujaji na wageni waliofurika katika Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro hapa Vatican, aliutumia muda huo, kuomba amani kwa taifa la Syria, ambako watu wanaendelea kuishi katika hali za vitisho vya ukatili mkubwa wa machafuko ya wenyewe kwa wenyewe, na hasa mwelekeo wa kufumka wa wimbi jipya la vita.

Papa alitoa wito huo huku akionyesha kuguswa na hali hiyo ya mateso na wasiwasi mkubwa kwa watu wa Syria, ambako katika kipindi hiki cha miaka miwili na nusu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, zaidi ya watu 100 elfu kati yao elfu 7 wakiwa watoto wamepoteza maisha yao. Na zaidi ya millioni 4 kwa wakati huu wanaishi kama wakimbizi ndani ya nchi yao na nje ya nchi.

Katika hali hiyo ya masikito Papa alisema,” kwa mara nyingine, nalazimika kupaza sauti yangu nikiwaomba wote wale wanao husika na ghasia hizi,wasikilize kilio cha watu wasiokuwa na hatia na wasitishe ukatili huo unaoendelea kutesa na kudhulumu watu kwa ghasia za mapigano na hasa matumizi ya silaha kali, kushambuliana ndugu kwa ndugu, kama inavyo elezwa na kushuhudiwa katika vyombo vya habari.
Papa ameasa, kuongezeka kwa ghasia za wenyewe kwa wenyewe hakuwezi kutoa jibu la uwepo wa matumaini katika mustakhabali wa taifa , njia pekee ya kupata ufumbuzi katika tofauti zao ni kupitia njia ya majadiliano , mmoja akisikiliza uzito wa hoja ya mwingine katika hali ya amani na maridhiano, na kuona jinsi wanavyoweza kusawazisha tofauti hizo kwa makubaliano.

Papa alionyesha ukaribu wake kupitia sala na msaada wa kihali unaotolewa daima, na vyombo vya misaada vya Kanisa kwa wahanga wote wa vita hii, na kwamba, anafuatilia kwa makini kinachoendelea Syria na hasa hali ya wakimbizi na watoto, na daima anawasihi wasikate tamaa bali waendelee kudumu katika tumaini la amani

Na aliigeukia jumuiya ya Kimataifa, akiitaka ionyeshe uwajibikaji zaidi katika juhudi za kusitisha ukatili unaoendelea Syria , na wakati huohuo, itoe msaada si tu wa kihali lakini hawa katika upatikanaji wa jawabu sahihi la kusitiza vita inavyoendelea kufanya uharibifu na mauaji.

Na mwisho alitoa mwaliko kwa watu wote kutolea sala zao kwa Malkia wa amani .Yesu ni njia pekee ya wokovu

Mapema kabla ya kutoa wito huu , Papa alirejea masomo ya Jumapili, hasa juu ya somo la Injili, na kutoa maelezo kwamba, maneno ya Yesu katika Injili iliyosomwa, yanaasa watu kwamba kuingia katika ufalme wa Mungu si mzaha au lelemama, bali ni kuzingatia amri za Mungu , na hivyo unakuwa ni mlango mwembamba, kwa maisha ya yasiyofuata amri za Mungu.
Yesu alizungumzia juu ya Mlango Mwembamba, wakati akijibu swali ni wagapi wataokolewa. Alisema cha msingi si idadi ya wataookolewa lakini hasa ni kuijua ni ipi njia ya wokovu.
Yesu mwenyewe ndiye njia pekee ya wokovu. Yesu yule aliye jitolea mhanga msalabani na kufufuka, aliyeyakubali mateso yote, ili binadamu pia apate kusamehewa dhambi zake ili aingie katika nyumba ya Bwana. Ni kuingia katika Ufalme wa Mungu na kuishi katika usharika pamoja nae. Mlango huo mwembamba ni kumkiri Yesu Mwenyewe, kuwa njia ya uzima wa milele.
Papa alisisitiza mlango huu wa Yesu daima ni wazi kwa kila anayeamini , na kamwe haufungwi . Ni mlango wazi kwa kila binadamu , mlango usiojua kubagua au kuwa na upendeleo , ni mlango wa ajabu wenye kuwapokea waamini wote.All the contents on this site are copyrighted ©.