2013-08-26 10:05:40

Mshikamano na Wakristo wanaodhulumiwa nchini Misri


Baraza la Maaskofu Katoliki Uswiss linapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati kwa Wakristo wanaoishi Misri na Mashariki ya Kati, wakati huu wanapokabiliana na hali ngumu ya maisha kutokana na vita, vurugu na kinzani za kijamii zinazoendelea kusababisha maafa makubwa katika maeneo haya.

Maaskofu wa Uswiss wanasema, Wakristo nchini Misri wanaishi katika mazingira hatarishi na kwamba, Kanisa nchini Uswiss linaungana na waamini wanaodhulumiwa na kunyanyasika kutoka na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, ili waweze kupata ujasiri wa kusonga mbele pasi na kukata tamaa. Jumamosi na Jumapili iliyopita, Baraza la Maaskofu Katoliki Uswiss limetolea Ibada za Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wananchi wanaoishi Misri na Mashariki ya Kati hususan nchini Syria, ili waweze kupata amani na utulivu kwa njia ya majadiliano ya kweli.

Kanisa Katoliki nchini Uswiss limetolea Ibada ya Misa kwa ajili ya wote wanaoendelea kudhulumiwa na kukosewa haki, ili mioyo ya watu wengi zaidi iweze kumwongokea Mwenyezi Mungu ambaye ni chemchemi ya amani na upendo. Vita inasababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Ni jambo la kusikitisha kuona kwamba, nyumba za Ibada, Miundo mbinu ya elimu, afya na maendeleo ya Jamii inaharibiwa kwa chuki zisizo na msingi.

Maaskofu wa Uswiss wanasema kwamba, inatia moyo kuona kwamba, waamini wengi wa dini ya Kiislam wanaguswa na kusikitishwa na vitendo vya dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo. Hizi ni dalili njema kwamba, bado kuna uwezekano wa kuishi kwa amani na utulivu, kila mtu akiheshimu na kuthamini dini na imani ya jirani zake.

Maaskofu wanaendelea kuungana na watu wenye mapenzi mema kuitaka Serikali ya Misri kutafuta ufumbuzi wa machafuko ya kisiasa nchini humo kwa njia ya kidiplomasia na majadiliano kwa kuheshimu na kuthamini uhuru wa kidini. Baraza la Maaskofu Katoliki Uswiss linapanga kupeleka msaada wa hali na mali kwa njia ya Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki, Caritas.
All the contents on this site are copyrighted ©.