Machafuko ya kisiasa nchini Misri, wakristo wanaendelea kunyanyasika zaidi!
Askofu Kyrillos William Samaan wa Jimbo Katoliki la Assiut katika mahojiano na Shirika
la Kipapa la Misaada kwa ajili ya Makanisa hitaji anasema kwamba, machafuko ya kisiasa
nchini Misri yaliyowaka moto hapo tarehe 3 Julai 2013 kwa kumwondoa madarakani Rais
Mohamed Mursi kwa njia za kijeshi, kumepelekea Wakristo wengi kudhulumiwa.
Baadhi
ya Waislam wenye msimamo mkali wanadhani kwamba, hizi ni njama za Wakristo kutaka
kutawala Misri. Mwelekeo huu potofu wa kudumaa kwa demokrasia ya kweli, utawala wa
sheria na uhuru wa kuabudu, kumepelekea Wakristo kuanza kunyanyaswa kana kwamba, wao
ndio chanzo cha machafuko ya kisiasa nchini Misri.
Inasikitisha kuona kwamba,
kuna baadhi ya Waamini wanatumia machafuko ya kisiasa nchini Misri kwa kuchoma nyumba
za ibada na miundo mbinu ya huduma msingi za kijamii jambo ambalo ni hatari sana kwa
maisha na ustawi wa wananchi wa Misri kwa siku za baadaye. Kutokana na mwelekeo wa
sasa, Wakristo ndio wanaoendelea kulipia gharama ya machafuko ya kisiasa nchini Misri.
Kuna
haja kwa Waislam na Wakristo kujenga utamaduni wa majadiliano ya kidini, ili kwa pamoja
waweze kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya uhai, mafao ya wengi, demokrasia
na utawala wa sheria unaoheshimu uhuru wa kuabudu na kwamba, raia wote wa Misri wana
haki sawa na wala hakuna raia wa daraja la pili kutokana na imani yake.
Kinzani
na madhulumu yanayojitokeza miongoni mwa wananchi wa Misri yanahitaji upatanisho na
msamaha wa kweli unaopata chimbuko lake kutoka katika undani wa moyo wa mwamini mwenyewe.
Wananchi wote wa Misri washirikiane kwa pamoja ili kufanya mabadiliko ya dhati yatakayozingatia
mafao ya wengi nchini Misri pamoja na kutetea haki msingi za binadamu.