Changamkieni Uinjilishaji wa kina kwa furaha na unyofu wa moyo!
Pamoja na kwamba wanadamu hawana mazoea sana ya kuchangamkia na kufanikisha mambo
ya wengine, Mapadri wachangamkie kwa furaha na unyoofu uinjilishaji kama vile Yohane
Mbatizaji alivyomshabikia Kristo na kuwatambulisha wanafunzi wake kwa Kristo. Hayo
ameyasema Askofu Mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Mwanza, mwishoni mwa
Juma, katika adhimisho la Misa Takatifu katika Parokia ya Mtakatifu Kizito Kabila,
Jimbo kuu la Mwanza, ambapo alitoa daraja takatifu la Upadre kwa Shemasi Peter Madata. Padri
Peter Madata ameonesha nia yake dhahiri na kwa uhuru ili kumtumikia Mungu katika ukuhani
wa huduma. Askofu Mkuu Ruwa’ichi kamualika azingatie nia yake hiyo pamoja na masharti
yanayoambatana na maisha ya Upadri. Masharti hayo ni pamoja na useja. Amemuonya kuwa
makini na walimwengu wanaoshabikia kuwa useja ni uvunjifu wa haki za binadamu na uonevu,
na badala yake atambue kuwa Useja ni kukumbatia Kanisa na kudhihirisha Ubaba wa Padri
kwa wana Kanisa, amesema Askofu Mkuu Ruwa’ichi. Masharti hayo ni pamoja na maisha
ya ufukara, kutokujilimbikizia mali, hivyo Padri mpya Peter Madata kaalikwa kuwa mtiifu
na kuhudumia vema na kwa moyo wa ukarimu popote atakapotumwa hata mahali anapodhani
kuwa hakuna mshiko wa kutosha wala mnuso wa kuridhisha. Akiwa mwaminifu na mwadilifu
hatakuwa tajiri lakini pia hatapungukiwa chochote, hivyo ajitose zaidi katika kulijenga
Kanisa la Kristo. Askofu Mkuu Ruwa’ichi anawaalika mapadri wote kuvaa silaha za
kimungu katika utume wao: ukweli wa kauli na ukweli wa nafsi uwakoleze mapadri na
kuwaongoza; watende haki kwa kumpa kila mmoja anachostahili ikiwa ni pamoja na kuzingatia
kuwahi katika maadhimisho; wawe na bidii ya utume kwa ukunjufu na ukomavu; Neno la
uzima walitafakari, waliishi na kulifundisha na hivyo, wasijiridhishe na mambo ya
kijiweni na udaku; wajikite katika sala ili Mungu abariki, aongoze, asindikize na
kufanikisha mipango yao na kila wafanyacho. Askofu Mkuu Ruwa’ichi amemwalika Padri
Peter Madata aambatane na Bikira Maria katika utume wake kwa kumtambua kuwa ni Mama
yake na mama wa Kanisa. Kawaalika pia wanajimbo wote kuziombea parokia zote za Jimbo
kuu la Mwanza zizidi kuzaa na kulea miito mitakatifu.
Na Padre Agapito Mhando. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.