2013-08-24 10:59:09

Kanisa linafuatlia machafuko ya kisiasa nchini Misri kwa uchungu na matumaini!


Patriaki Ibrahim Isaac, Rais wa Baraza la Mapatriaki na Maaskofu nchini Misri anasema kwamba, Kanisa linaendelea kufuatilia matukio ya kigaidi, mauaji ya watu wasiokuwa na hatia na uharibifu wa miundo mbinu kwa uchungu mkubwa na matumaini kwamba iko siku, utawala wa sheria utaweza kushika hatamu na amani kutawala tena nchini Misri.

Kanisa linaunga mkono juhudi zote zinazofanywa na vikosi vya ulinzi na usalama kwa ajili ya masilahi ya taifa na kwamba, wasingependa kuona watu wanaingilia masuala ya ndani ya Misri. Wanavishukuru vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa vinavyotekeleza dhamana yake kwa kuzingatia kanuni, maadili na sheria za kazi, ili kubainisha ukweli wa mambo.

Kanisa linawashukuru waamini wa dini ya Kiislam waliojitoa mhanga kwa ajili ya kulinda na kutetea maisha ya viongozi wa Kanisa na Makanisa yaliyokuwa hatarini kuchomwa moto.

Viongozi wa Kanisa wanapenda kuwajulisha walimwengu kwamba, kuna mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi nchini Misri na wala hii si vita ya kidini kama wengi ambavyo wanapendwa kusadikishwa. Wanatuma salam za rambi rambi kwa wote walioguswa na machafuko ya kisiasa nchini Msiri.







All the contents on this site are copyrighted ©.