Jifunzeni kutoka kwa Papa Francisko katika kuwahudumia watu wenu!
Askofu mkuu Joseph Coutts wa Jimbo kuu la Karachi na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Pakistan anasema, unyenyekevu unaooneshwa na Baba Mtakatifu Francisko ni amana kubwa
inayoweza kusaidia kuleta mabadiliko katika maisha na utume wa Kanisa na Jamii katika
ujumla wake.
Askofu mkuu Coutts ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa anazungumza
na wanataaluma, wakurugenzi pamoja na viongozi wa kisiasa nchini Pakistan. Anasema,
viongozi mbali mbali wanayo mengi ya kujifunza kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko
katika mchakato wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga
dunia inayosimikwa katika misingi ya haki, amani na upatanisho wa kweli, vielelezo
msingi katika maisha ya Mtakatifu Francisko wa Assisi.
Baba Mtakatifu ni kiongozi
anayeonesha dira kwamba, uongozi ni huduma kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii. Uongozi ni kielelezo cha upendo na mwaliko wa kujenga utamaduni
wa kusikiliza na kuwajali wengine katika shida na mahangaiko yao ya ndani.
Ikiwa
kama viongozi katika medani mbali mbali za maisha watajifunza kusikiliza na kuhudumia
kwa makini, jamii nyingi zinaweza kuonja mabadiliko ya kweli kutoka katika undani
mwao!